Mahakama yaamuru aliyemwibia mwajiri wake arejeshwe nchini

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imemuamuru Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Ilala, kuanza na kukamilisha uchunguzi wa malalamiko ya wizi yaliyowasilishwa ofisini kwake na Radhika Pankanj dhidi ya aliyekuwa mfanyakazi wake (Mukesh Menaria).

Aidha, imeelekeza kuchukua hatua zote halali na zinazofaa ili kuwezesha uchunguzi huo na kuhakikisha Mukesh anarudi nchini ili kukamilisha uchunguzi huo.

Radhika anadai Mukesh alimuibia vitu mbalimbali ikiwemo bangili ya dhahabu, pete (emerald ring), saa aina ya Chaumet na bangili ya almasi, zinazokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi Dola za Marekani 150,000 (takriban Sh376 milioni).

Mahakama hiyo imetoa amri hizo katika maombi yaliyofunguliwa na Radhika dhidi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) Ilala pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Uamuzi huo umetolewa Agosti 25, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga, aliyekuwa akisikiliza maombi hayo.

Katika maombi hayo Radhika alikuwa anaiomba mahakama kumlazimisha RCO Ilala kuhitimisha upelelezi wa malalamiko yaliyowasilisha katika ofisi hiyo yenye namba CDS/IR/2104/2024.

Zaidi ya hayo, mwombaji huyo anaomba amri inayoelekeza RCO Ilala kuchukua hatua zote muhimu na halali ili kufanikisha Mukesh kukamatwa na kurejeshwa nchini ili kuwezesha kukamilika kwa haraka kwa upelelezi wa suala hilo pamoja na amri nyingine.

Mahakamani hapo imeeelezwa kuwa Radhika ambaye ni raia wa Cyprus anayeishi Uswizi, anayejishughulisha na biashara maeneo mbalimbali ikiwemo London, Uswizi, Tanzania, India, na Uganda.

Anafanya shughuli hizo za biashara kupitia mashirika kadhaa, ambayo ni Bing Enterprises Limited, PRO Industries PTE Limited, na Vari Agro Tanzania Limited.

Kwa mujibu wa Radhika, masilahi yake ya kibiashara yanahusisha sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kilimo, viwanda, biashara ya kimataifa, madini na usindikaji wa mazao ya kilimo.

Agosti 2024, alibaini baadhi ya vitu vya thamani vinavyomilikiwa na kampuni zake kutokuwepo, alianza uchunguzi kupitia watumishi mbalimbali ambapo Mukesh alikiri kuchukua vitu kadhaa.

Hatua hiyo ilisababisha ukaguzi wa mali za Mukesh kufanyika na kusababisha baadhi ya vitu kupatikana huku vingine vyenye thamani ya zaidi Dola za Marekani 150,000 vikiwa havipo.

Septemba 30, 2024, Radhika aliwasilisha taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam, akiomba hatua stahiki za uchunguzi na kisheria zichukuliwe.

Kumbukumbu za maombi hayo zinaonyesha kuwa kwa barua ya Oktoba 16, 2024, yenye kumbukumbu namba GW/RPO/01/01/16/10/2024 na kupitia kwa mawakili wao, aliuliza kuhusu maendeleo ya jalada la uchunguzi

Baadaye, kwa barua ya Oktoba 17, 2024 yenye kumbukumbu namba BD.476/838/01A/220, ofisi ya RCO Ilala ilimtaarifu Radhika kuwa Mukesh amekamatwa na Polisi Oktoba 4, 2024 mkoani Kagera ambapo alisafirishwa hadi Dar es Salaam kwa mahojiano na uchunguzi.

Baada ya kujulishwa hivyo, Radhika alienda Kituo cha Polisi kuuliza kuhusu upelelezi na hatua nyingine za kisheria ambapo aliruhusiwa kuonana na Mukesh na polisi walimhakikishia kuwa angeendelea kuwa chini ya ulinzi kulingana na matakwa ya kisheria.

Radhika amedai kuwa baada ya kuona ucheleweshaji na ukimya wa muda mrefu kuhusiana na suala hilo na alipoenda kituoni hapo kufuatilia maendeleo ya upelelezi alibaini Mukesh aliachiwa kwa dhamana  na kutorokea nje ya nchi.

Kufuatia hali hiyo Radhika alioma kibali cha kuwasilisha maombi hayo akidai RCO Ilala kutochukua hatua na kushindwa kumdhibiti mtuhumiwa jambo ambalo linapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kurejesha mali zake za thamani kubwa ambazo zinaa uhusiano mkubwa na familia yao.

Mdaiwa huyo wa kwanza (RCO Ilala), alipinga maombi hayo akidai kuwa Polisi walianza uchunguzi, ambapo ilibainika kuwa Radhika na Mukesh walikuwa wameingia katika makubaliano ya suluhu na kwa mujibu wa masharti ya mkataba, pande zote ziliridhia pamoja na mambo mengine, kuondoa madai hayo ya wizi.

Mjibu maombi huyo alidai kuwa bila kujali makubaliano ya suluhu kati yao, Polisi waliendelea na uchunguzi na baadaye ilibainika kuwa hakuna ushahidi uliothibitisha madai ya wizi ya Radhika  dhidi ya Mukesh ambaye aliachiwa kwa dhamana.

Amedai kuwa Mukesh hajaikimbia nchi na  badala yake, alikabidhiwa kwa Interpol Uganda kama mwathirika wa biashara haramu ya binadamu, na kuna uchunguzi unaoendelea nchini Uganda.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo uliofanyika kwa njia ya maandishi, Radhika aliwakilishwa na Wakili Lucky Mgimba huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili Francis Wisdom.

 Jaji Mwanga amesema kwa maoni yake tangu Radhika awasilishe malalamiko yake kumekuwa na ucheleweshaji wa upelelezi kwa madai ya kutokuwa na ushahidi na kuwa hata madai ya RCO Ilala kuwa Wakili wa Radhika alijulishwa kufungwa kwa upelelezi bado halijathibitishwa kwani hakuna uthibitisho wa hilo.

Amesema pia hakuna uthibitisho unaoonyesha iwapo jalada la uchunguzi lilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na maelekezo zaidi.

Jaji Mwanga amesema zaidi ya hayo, madai kwamba mtuhumiwa alikabidhiwa kwa mamlaka ya Uganda na kuwa hakuna ushahidi thabiti wa kuthibitisha madai hayo.

“Kushindwa huko ni kutofuata taratibu na kutotendea haki, kwani mwombaji alikuwa na haki ya kufahamishwa matokeo ya uchunguzi, ikiwa ni pamoja na uamuzi wowote wa kufunga jalada. Ingawa mjibu maombi anadai kuwa upelelezi ulikamilika kwa kuzingatia mazingira yaliyoainishwa hapo juu, ukamilishaji huo haukuwa wa kiutaratibu,” amesema.

Jaji amesema kuhusu sharti la kuzingatia kama mwombaji (Radhika) ana masilahi ya kutosha ya kisheria au binafsi kwa kuonyesha kwamba anaathiriwa moja kwa moja na hatua au kutochukua hatua kwa mujibu maombi na kwamba suala hilo linahusu wajibu wao wa kisheria.

Jaji Mwanga amesema katika maombi hayo Radhika analalamikia RCO Ilala hakuchukua hatua na kushindwa kumdhibiti mtuhumiwa, jambo ambalo limepunguza kwa kiasi kikubwa matarajio ya kurejesha vitu vilivyotajwa vyenye thamani kubwa ya fedha.

“Ikizingatiwa kuwa baadhi ya vitu vilivyoibiwa ni mali ya Mwombaji na baadhi ya kampuni yake, anaguswa moja kwa moja na upotevu huo,” amesema.

Baada ya Mahakama hiyo kukubali maombi hayo, ilitoa amri nne ambazo ni kumlazimisha RCO Ilala kuanza tena na kukamilisha uchunguzi wa malalamiko hayo kwa mujibu wa sheria.

Nyingine ni RCO Ilala kuelekezwa kuchua hatua zote halali na zinazofaa kuwezesha uchunguzi huo na kuhakikisha Mukesh anarudi katika mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amri nyingine ni ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya amri hiyo, RCO Ilala anapaswa kumpatia Radhika au Wakili wake taarifa ya maandishi kuhusu maendeleo na hali ya upelelezi, ikijumuisha hatua yoyote iliyochukuliwa katika kumtafuta mtuhumiwa na kurejesha vitu vinavyodaiwa kuibiwa.