KOCHA Mkuu wa KMC, Marcio Maximo amesema kikosi chake kiko fiti kwa asilimia kubwa na kinachoendelea ni kutengeneza mbinu zitakazokipa matokeo mazuri mapema mwezi ujao ligi itakapoanza.
KMC imerejea kwenye uwanja wa nyumbani baada ya kuweka kambi ya wiki mbili Zanzibar huku kocha huyo akidai kuwa maandalizi kwa ujumla yanakwenda vizuri na anaridhishwa na uwezo wa wachezaji.
Akizungumza na Mwanaspoti muda mfupi baada ya mazoezi, mkufunzi huyo alisema timu inaendelea vizuri na wachezaji wana vipaji vikubwa ilhali anachokifanya sasa ni kutengeneza mbinu sahihi ambazo zitawapa matokeo.
“Nafurahishwa na juhudi za wachezaji mpango sahihi uliopo ni namna ya kupeana mbinu sahihi za kupata matokeo kuhusu vipaji na uwezo nina wachezaji wengi bora na umri wao unaruhusu kufanya mambo makubwa ndani ya timu hii,” alisema na kuongeza:
“Nafahamu ligi ilivyo ngumu na pia naona wapinzani wanavyosajili mikakati inaendelea vuizuri tunafanya kile ambacho tunaamini kitatoa picha nzuri ya ushindani msimu utakapoanza.”
Akizungumzia utimamu, kocha huyo alisema wachezaji wote wapo sawa kutokana na kuanza pamoja maanadalizi na kuzingatia kile anachowafundisha.
Akizungumzia soka la Tanzania, alisema analifahamu na alikuwa analifuatilia hivyo anajua nini afanye ili aweze kuendana na kasi ya ushindani huku akisistiza kuwa hatarajii mteremko kwani malengo ni kuwa sehemu ya timu shindani msimu unapoanza ili kufanya vizuri kwenye ligi.
“Ligi ambayo ni bora haiwezi kuwa na timu dhaifu naamini kutakuwa na ushindani mkubwa najipanga kwa kuiandaa timu iwe shindani na kuwa bora kwa kuendana na kasi ya wapinzani.”