Lindi. Wakati matukio ya ajali za moto yanayohusisha watoto yakiendelea kuripotiwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limesema kuanzia Januari hadi Agosti 2025, kumeripotiwa matukio 10 tofauti.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Alhamisi, Agosti 28, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori amesema matukio ya ajali za moto yamekuwa yakijirudia mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto wao wanapowaacha nyumbani wakienda kwenye shughuli zao.
Pia, ameeleza kuwa endapo itabainika kuwepo kwa uzembe wa wazazi au walezi uliochangia ajali hizo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Vifo vya watoto vimekuwa vingi sana, Februari kulitokea vifo vya watoto wanne wa familia moja Wilaya ya Nachingwea, wamefariki dunia baada ya nyumba yao kuungua moto, Julai katika Wilaya ya Ruangwa walifariki dunia watoto watatu wa familia moja kwa kuungua na moto, Agosti 26, 2025 wamefariki dunia watoto wawili wa familia moja kwa kuungua na moto wilayani Lindi,” amesema Kamanda Imori.
Amesema kifo kingine kimetokea Agosti 27, 2025 saa 2:50 asubuhi katika Kijiji cha Matandu kata ya Kivinje Wilaya ya Kilwa ambapo nyumba ya Mbukwa Jongoo (48) iliungua moto na kusababisha kifo cha mtoto wake Rashid Jongoo (1) aliyekuwa amelala ndani huku wazazi wake wakiwa shambani umbali wa kilometa tatu.
“Mtoto alikuwa amelala ndani wazazi wamekwenda shambani umbali wa kilometa tatu na kuacha moto ukiwa ndani bila kuzimwa, moto huo uliunguza nyumba,” amesema Imori.
Amesema mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Kinyonga Wilaya Kilwa na kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
“Nitoe wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na usalama wa watoto wao, hasa wanapokuwa wamelala au wanapoachwa peke yao bila uangalizi wa mtu mzima. Ni bora kuwaachia watoto kwa jirani unayemuamini au mtu mwingine mwenye uwezo wa kuwalinda, kuliko kuwaacha nyumbani pekee na kuondoka,” amesema Kamanda Imori.
Aidha, amewataka wazazi kuacha mara moja tabia ya kuwasha moto ndani ya nyumba na kuondoka bila kuhakikisha moto huo umezimwa, kwa kuwa ndio sababu kubwa ya ajali zinazogharimu maisha ya watoto.
Kamanda Imori amesema chanzo cha tukio la kifo cha mtoto mmoja hivi karibuni ni moto uliosababishwa na jiko lililoachwa likiwaka ndani ya nyumba ya nyasi, wakati mtoto huyo akiwa amelala.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limesema limejipanga kuimarisha ulinzi na usalama kwa kiwango cha juu kuelekea kampeni na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 na kuwataka wananchi kuondoa hofu.
“Wananchi wa Mkoa wa Lindi msiwe na wasiwasi wowote. Mkoa uko salama. Tumejipanga ipasavyo kuhakikisha hakuna uvunjifu wowote wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Ulinzi utaimarishwa wakati wote,” amesema Kamanda Imori.