Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kupigania haki, amani ya kweli na utulivu, mambo ambayo wananchi wote wanayahitaji kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema sauti ya viongozi wa dini ina uzito mkubwa na ndio msingi wa kudumu wa kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Kauli hiyo ameitoa leo, Alhamisi Agosti 28, 2025, alipokutana na kufanya mazungumzo na Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Mhashamu Augustine Shao, katika ofisi za jimbo hilo zilizopo Kanisa la Mtakatifu Joseph, Minara Miwili, Shangani Unguja.
Katika mazungumzo hayo, Othman pia amepokea ripoti maalumu kuhusu hali ya kisiasa nchini na nafasi ya ACT-Wazalendo katika harakati za kudumisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Amesema viongozi wa dini ni alama ya hekima, umoja na mshikamano, hususan kwa Zanzibar na kusisitiza kuwa hitaji la sasa ni kuhakikisha nchi inaelekea kwenye uchaguzi kwa amani na haki.

“Sisi ACT-Wazalendo tumefanya jitihada nyingi kutafuta amani ya kudumu, ikiwamo kukubali kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa licha ya uchaguzi wa 2020 kuacha makovu makubwa kwa wanachama wetu na wananchi,” amesema Othman.
Amefafanua kuwa dhumuni kuu la Serikali ya Umoja wa Kitaifa lilikuwa kujenga mazingira ya maridhiano na mashirikiano ili kuondoa misuguano ya kisiasa visiwani, lakini baadhi ya makubaliano bado hayajatekelezwa.
Miongoni mwa mambo aliyoyataja ni kura ya mapema, kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi na mauaji ya wananchi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Pia amesema upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari mkazi kwa waliopokonywa haki hiyo kisheria, pamoja na kurejesha imani ya wananchi kwa uchaguzi huru na wa haki kwa kuondoa wasimamizi waliotuhumiwa kuhusika na matukio hayo ya maafa.
Amesisitiza kuwa dhamira ya chama hicho si kupata vyeo, bali kudumisha amani ya kweli na maendeleo endelevu ya nchi.
“Viongozi wetu tuliwahi kukutana na Rais wa Zanzibar na kumpa ahadi ya kushirikiana naye, lakini kwa sharti la kuhakikisha matakwa ya wananchi yanatekelezwa. Hata hivyo, inaonekana suala hilo limepuuzwa,” amedai Othman.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema maendeleo ya Taifa hayawezi kupatikana bila kusimama kwenye misingi ya haki na amani.
“Si vyema kamati za amani zikawa za kuzima moto mwishoni, bali ni lazima sasa zisimamie na kupaza sauti mapema juu ya mambo yanayoweza kuvuruga utulivu,” amesema Jussa.
Naye Askofu Shao ameeleza kuwa amani ya kweli hujengwa pale kila mtu anapopata haki yake.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekuwa mlango wa amani na utulivu na imechangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kupitia utalii. Hivyo ni lazima haki na amani viheshimiwe, kwani bila hivyo kinachobaki ni hofu iliyojificha,” amesema Askofu Shao.