Opah anaendeleza uthubutu kwa wanawake

BAADA ya kutumikia timu ya wanawake ya FC Juarez kwa msimu mmoja, juzi nahodha wetu wa Twiga Stars, Opah Clement alijiunga rasmi na SD Eibar ya Hispania.

Ni uhamisho ambao hapa kijiweni umetufurahisha sana kwa vile kwanza anaenda katika nchi ya kisoka hasa ambayo ina moja kati ya ligi bora za soka za wanawake.

Baadhi wanaweza kuhisi Hispania inatamba katika soka la wanaume tu lakini hata kwa wanawake ni wa moto sana na wamekuwa wakifanikiwa kwa timu zao za taifa na hata klabu zao.

Iko wazi Hispania siyo nchi rahisi kwa mchezaji wa kigeni kuingia na kwenda kucheza soka la kulipwa tena hasa akiwa hajazaliwa na kukulia Ulaya, hivyo kwa Opah hayo ni mafanikio makubwa na yanayohitaji pongezi.

Lakini kingine ni angalau sasa Opah atapata nafasi ya kucheza tofauti na alivyokuwa kule Juarez ambako hakupewa nafasi kubwa ya kucheza katika Ligi Kuu ya Wanawake ya Mexico jambo ambalo kiukweli hatukuwa tunalipenda.

Kwa upande mwingine usajili wa Opah unatukosha kwa sababu umeonyesha uthubutu ambao wanasoka wa kike wa Tanzania wamekuwa nao kwa muda mrefu wa kwenda nje kusaka malisho bora zaidi kuliko yale wanayoyapata hapa.

Ilianzia miaka hiyo ambapo dada zao kina Sofia Mwasikili walijitosa na kwenda kucheza soka la kulipwa nje japo kwa uchache na baadaye wakaibuka kina Mwanahamisi Omary Gaucho.

Leo hii tuna mastaa kibao ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya Tanzania na wamekuwa na mchango mkubwa kwa Twiga Stars yetu hadi tunaona inaweza kushindana na timu zenye mafanikio na historia kubwa ya soka la wanawake Afrika.

Ukimtoa Opah wapo kina Clara Luvanga, Diana Lucas, Enekia Kasonga, Noela Luhala, Maimuna Kaimu, Suzan Adam, Hasnath Ubamba na Malaika Meena.