TBS YATOA ELIMU YA UDHIBITI UBORA KWENYE MAONESHO YA WIKI YA USTAWI WA JAMII

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake katika Maonesho ya Wiki ya Ustawi wa Jamii, likiwa na lengo la kuhakikisha jamii inatumia bidhaa zinazokidhi matakwa ya Sheria za Viwango na hivyo kupata huduma bora.

Akizungumza leo Agost 28,2025 Jijini Dar es Salaam kwenye Maonesho hayo, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TBS, Bi. Nuru Meghji, amesema shirika hilo limekuwa likitoa elimu kuhusu majukumu yake makuu ambayo ni pamoja na kutunga na kusimamia viwango, kudhibiti bidhaa, kuthibitisha ubora wa bidhaa, kusajili bidhaa za vyakula na vipodozi vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi, pamoja na kutoa huduma za vipimo na uegaji.

Ameeleza kuwa TBS imejipanga vyema kupitia maabara zake mbalimbali zinazotoa vipimo vya bidhaa tofauti. “Tunayo maabara za bidhaa za chakula, vipodozi, kemikali, chuma, umeme, ujenzi, vifungashio na nguo. Hii inatoa fursa ya kupima viwango vya bidhaa zinazozalishwa kwenye makundi yote haya,” amesema

Aidha, amesema shirika hilo limekuwa likifanya ukaguzi wa bidhaa katika viwanda nchini pamoja na bandarini ili kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia au zinazozalishwa nchini zinakidhi matakwa ya Sheria za Viwango kwa kuzingatia ubora na usalama wa mlaji.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupata huduma za TBS bure, hatua inayolenga kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika kufikia viwango vya ubora wa bidhaa.

“Hii ni fursa kubwa kwa wajasiriamali wadogo kuondoa visingizio na kuhakikisha bidhaa zao zina ubora unaokubalika,” amesisitiza.

Maadhimisho ya Wiki ya Ustawi wa Jamii kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Pata Msaada wa Kisaikolojia, Imarisha Afya ya Akili.”