KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano, huku ikielezwa nahodha wa zamani wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyetua klabuni hapo kwa kishindo amempora mtu namba mapema.
Tshabalala ni kati ya wachezaji watano wa Yanga waliokuwa katika timu ya taifa iliyokuwa ikishiriki Fainali za CHAN 2024 ambao walipewa mapumziko mafupi kabla ya kuungana na wenzao kwa mechi ya Kilele cha Wiki ya Wananchi itakayofanyika Septemba 12 kwenye Uwanja wa Mkapa.
Pia Yanga inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii ya kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba itakayopigwa Septemba 16 kabla ya kuanza majukumu ya mechi za kimataifa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa kuumana na Wiliete Banguela ya Angola ugenini.
Lakini, kabla ya kutua mazoezini kuungana na wenzake, beki mpya wa kushoto, Tshabalala imedaiwa ameichukua namba 15 iliyokuwa ikivaliwa na beki wa kulia wa timu hiyo, Kibwana Shomari.
Imethibitishwa kuwa, Tshabalala aliyezoeleka akivaa jezi hiyo kwa miaka 11 akiwa Simba na hata katika timu ya taifa, ameomba kuachiwa jezi hiyo, huku Kibwana akitafutiwa namba nyingine.
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta, Kibwana ambaye amethibitisha hilo. “Ni kweli nimemkabidhi jezi namba 15 ni kaka yangu yule sikuwa na namna yoyote, lakini hadi sasa sijajua nitavaa jezi namba ngapi nasubiri wao waamue wananipa namba ngapi,” alisema Kibwana aliyesajiliwa misimu mitatu iliyopita akitokea Mtibwa Sugar.
Tshabalala ametua Yanga akiwa mchezaji huru.
Kibwana ambaye enzi za kocha Nasreddine Nabi alikuwa akitumika pia kama beki wa kushoto, ameitumikia Yanga kwa misimu mitatu akipiga kazi chini ya makocha wanne tofauti.
Alikuwa chaguo la kwanza chini ya Nabi lakini alianza kupoteza namba chini ya Miguel Gamondi na sasa ameongezewa nguvu kwa kusajiliwa Tshabalala anayeenda kusaidiana na Chadrack Boka aliyekuwa tangu msimu uliopita.
Tshabalala alijiunga na Yanga hivi karibuni akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Simba kumalizika, amekabidhiwa jezi hiyo ambayo ameizoea na imekuwa kama utambulisho wake kwa mashabiki kwa muda mrefu.
Taarifa kutoka ndani ya kambi ya Yanga iliyopo Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam, zimebainisha kwamba Tshabalala amekabidhiwa jezi hiyo baada ya kuomba.