Tabora. Wananchi wa Wilaya za Igunga na Nzega mkoani Tabora sasa wamepata ahueni baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara na madaraja mapya yaliyo chini ya mradi wa Rise unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), hatua hiyo imewaondolea kero ya usafiri na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii zilizokuwa zikikwamishwa na miundombinu duni kwa miaka mingi.
Sehemu ya barabara hizo ni barabara ya Mbutu–Isakamaliwa yenye urefu wa kilomita 31.8, iliyojengwa kwa kiwango cha changarawe chini ya programu ya Bottleneck inayoendeshwa kupitia mradi wa Rise na Tarura kwa ufadhili nafuu wa Benki ya Dunia, ambapo awali ilikua changamoto kupitika na kukwamisha shughuli za maendeleo kwa sasa imekuwa mkombozi kwa wananchi wa Igunga na Kishapu ilibidi kuzunguka umbali mrefu, hali iliyowaletea changamoto kubwa hasa wakati wa mvua.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Agosti 27, 2025 Meneja wa Tarura wilaya ya Igunga, Mhandisi Aswile Mwasaga amesema ujenzi wa daraja hilo umetumia Sh496 milioni ambapo umekuwa msaada kwa wananchi wa Kishapu na Igunga.
“Kabla ya matengenezo hali ya upitikaji wa hii barabara haukua mzuri maana upitikaji wake ulikua ni wa shida hasa kwa wananchi kutoka Igunga kwenda Kishapu, wakati mwingine tulikuwa tunatumia zaidi ya saa moja kuzunguka ila kwa sasa tunatumia chini ya saa moja,’’ amesema Mhandisi Mwasanga.
Peter Pesambili ambaye ni mkazi wa Kata ya Isakamaliwa, Wilaya ya Igunga amesema licha ya matengenezo ya barabara hiyo ya Shinyanga boda inayounganisha Igunga na Kishapu zipo changamoto ikiwemo maeneo korofi ambayo mvua ikinyesha yanakua magumu kupitika.

“Kabla ya mradi huu kukamilika tulikuwa tunapata adha kubwa ila kwa sasa angalau, japo zipo changamoto ndogo ndogo ambazo zikifanyiwa kazi itakuwa nzuri zaidi ikiwemo sehemu ya barabara hii mvua ikinyesha ni panapitika kwa shida,’’ amesema Pesambili.
“Babarara hii imetusaidia sana hasa wananchi wa Isakamaliwa na Kishapu hasa kipindi cha mavuno kuvusha mazao na kuvusha mifugo yetu, limekuwa msaada mkubwa,” amesema mkazi Rehema Yakobo.
Mbali na barabara hiyo, mradi wa RISE umejumuisha ujenzi wa madaraja madogo yaliyokuwa kikwazo kwa muda mrefu. Miongoni mwao ni Daraja la Kasera lenye urefu wa mita 12 lililopo kwenye barabara ya Isese–Kasera–Mwamala, linalounganisha Kata za Mwangowe na Kasera.
Daraja hilo limekuwa msaada mkubwa kwani limewasaidia wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi na wanafunzi kuvuka kwenda shule bila matatizo.
Halmashauri ya Mji wa Nzega pia imefaidika na daraja la Ijanija lenye urefu wa mita 12, lililojengwa katika barabara ya Ijanija–Butandula. Daraja hili limeunganisha kata ya Ijanija iliyopo Wilaya ya Nzega Mjini na Kata ya Mwangowe, Nzega Vijijini na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.

Kaimu Meneja wa Tarura Wilaya ya Nzega, Mhandisi Faustine Mtungwa amesema daraja la la Ijanija lenye urefu wa mita 12 lilitengenezwa kwa thamani ya Sh120 milioni na limeokoa maisha ya wananchi wengi.
“Daraja hili lilitengenezwa kwa thamani ya Sh120 milioni mpaka ujenzi wake unakamilika lakini kabla ya hapo, mazingira haya yalikuwa magumu kwa sababu watu wengi wameenda na maji hilo ndio moja ya lengo kujenga daraja hili kwa uharaka,’’ amesema Mhandisi Mtungwa
Naye mkazi wa Kata ya Mwangowe, Halmashauri ya Nzega Vijijini, Richard Thomas amesema ujenzi wa daraja la Ijanija lenye urefu wa mita 12 umeondoa kero kubwa iliyokuwa ikiwasumbua kwa miaka mingi, ikiwemo kushindwa kuvuka mto nyakati za mvua.
“Ndugu zetu wagonjwa walikuwa hawawezi kufikishwa hospitali kwa wakati, hata wanafunzi walikwama. Lakini kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kujenga daraja hili, tunashukuru kwani sasa tunapita bila matatizo,” amesema.
Mradi wa RISE unatekelezwa nchini kwa lengo la kuboresha barabara za vijijini na kuondoa vikwazo vinavyosababisha wananchi kushindwa kunufaika na fursa za kijamii na kiuchumi kutokana na changamoto za miundombinu duni.
Hata hivyo, ujenzi wa barabara na madaraja mapya umekuwa suluhu yenye tija inayowezesha wananchi kusafiri kwa urahisi, kupunguza gharama za usafiri na kuongeza fursa za kibiashara na elimu.