Mashabiki na wa wananchama wa Simba Tawi la Mafinga na maeneo mbalimbali nje ya Mkoa wa Iringa, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi wa Wiki ya Simba Day unaotarajiwa kufanyika Agosti 30, 2025, wilayani Mufindi mkoani hapa, huku fursa ya kiuchumi ikitajwa kuwanufaisha.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 28, 2025 na Mwenyekiti wa Tawi la Simba Mafinga wakati Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu uzindulizi huo unaotarajiwa kufanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Wambi vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Mafinga.
Mkumbo amesema hadi sasa maandalizi kuhusu tukio hilo yanaendelea vizuri ambapo zaidi ya mashabiki na wanancha 1500 wanatarajiwa kuhudhuria huku fursa tatu zikitajwa.
“Hii ni bahati kwetu kuzinduliwa hapa Wiki ya Simba Day Kitaifa, hivyo mashabiki wote wa Simba wa Nyanda za Juu Kusini tunaomba kushirikiana ili kuunganisha nguvu katika tukio hili muhimu,” amesema Mkumbo.
Kwa upande wake mmoja wa Wanachama wa Simba Tawi la Mafinga, Peter Iranga amesema uzinduzi huo ni fursa kwa wananchi wa Mafinga kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kukuza kipato chao.
“Tunajivunia sisi kama Wanamafinga kwa uzinduzi wa Simba Day kufanyika hapa kwa sababu ni fursa nzuri kwetu hususani kwa akina mama wajasiriamali kuuza bidhaa zao kutokana na ujio huo mkubwa kwa wageni kutoka maeneo mbalimbali,” amesema Iranga.
Hata hivyo, Iranga amesema uzinduzi huo utawasaidia kukutana na watu tofauti kwa ajili ya fursa za kibiashara ukizingatia Mafinga wanajihusisha na biashara ya mazao ya misitu, hivyo wageni hao wataweza kujifunza biashara ya mbao kupitia tukio hilo.