Vijana chuo kikuu wabuni mradi kujiajiri wakiingiza kipato Sh133 milioni

‎Iringa. Katika mazingira yenye ushindani wa ajira na changamoto za kiuchumi, kikundi cha Vijana wa Iringa kimeanzisha mradi wa kisasa wa usindikaji mvinyo chini ya kampuni LordFather inayoundwa na Kassim Mgambo, Irene Mdegipala, Lukelo Mallumbo, Naomi Fedrick na Marry Mallumbo.

‎Akizungumza na Mwananchi Digital Agosti 27, 2025, Katibu wa Kampuni ya Lord father, Kassim Mgambo ameeleza kuwa kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 2020 na jumla ya wanafunzi watano wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), ikiwa na lengo la kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

‎”Mwaka 2021, kampuni ilisajiliwa rasmi na tukaanza uzalishaji wa mvinyo wa rozela kwa mtaji wa Sh150,000 na uwezo wa kuzalisha lita 150 kwa mwezi katika eneo la Kibwabwa A,” amesema Mgambo.

Muonekano wa ndani wa kiwanda cha usindikaji wa mvinyo katika halmashauri ya Manispaa ya Iringa. Picha na Christina Thobias

‎Kwa msaada wa mkopo wa Sh6.5 milioni

‎mwaka 2022 na uwekezaji wa ndani, uzalishaji uliongezeka hadi lita 750 kwa mwezi na mwaka 2023, kampuni ilifikia uzalishaji wa lita 3,000 kwa mwezi na bidhaa zake zikapata nembo ya ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

‎”Mnamo mwaka 2024, thamani ya mradi iliongezeka hadi Sh43 milioni na kufanikisha uanzishaji wa BML Foundation, shirika lisilo la kiserikali lenye lengo la kuwawezesha vijana wajasiriamali na zaidi ya vijana 160 walinufaika kupitia mafunzo, vifaa na ushauri wa biashara uliotolewa na shirika hilo,” amesema Mgambo.

Mgambo amesema kuwa juhudi hizo za kuwa na kiwanda cha usindikaji wa mvinyo zimewezeshwa pia na serikali kwa halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuwapatia mkopo wa Sh 70 milioni kutoka katika mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwezesha usindikaji wa mvinyo.

“Machi, 2025 tulifanikiwa kupata mkopo wa Sh70 milioni na huo umetuwezesha kufanya usindikaji katika kiwanda chetu,” amesema Mgambo.

‎Hata hivyo, Mgambo ameendelea kusema kuwa mwaka 2025, mradi huo ulihamia Mtaa wa Kitwiru B, Kata ya Kitwiru, na kufanikisha uzalishaji wa lita 12,000 za mvinyo kwa mwezi na bidhaa zinazozalishwa ni mvinyo wa rozela, nanasi na tangawizi, huku kampuni ikilenga kuzalisha lita 50,000 kwa mwezi ifikapo 2027.

‎Aidha Mgambo ameeleza kwamba kwa sasa, thamani ya mradi inakadiriwa kuwa Sh 133.8 milioni na masoko yake yameenea katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mbeya na Njombe kupitia mawakala huku wateja wakuu ni waandaaji wa sherehe, kumbi za starehe, maduka ya vileo na wanunuzi wa rejareja.

‎Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema kuwa mradi huo ni mfano wa utekelezaji wa sera ya viwanda na ajira kwa vijana.

‎”Serikali itaendelea kuwaunga mkono vijana kama hawa. Wameamua kubuni badala ya kutegemea ajira, na sasa wanakwenda kuwa waajiri,” amesema.

Ushauri wa Serikali kwa vijana

‎Akiwa kwenye ziara zake tofautitofauti mkoani Iringa, RC Kheri James ametembelea kuwataka vijana kutoogopa kuanza miradi midogo midogo yenye tija.

‎“Kila ajira kubwa huanza na wazo dogo. Vijana wajifunze kuthubutu, kushirikiana na serikali, na kutumia mikopo ya halmashauri. Msisubiri ajira za ofisini pekee,” amesisitiza RC James.

‎Aidha aliyekuwa Meya wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa hivi karibuni akizungumzia mkopo huo wa  asilimia 10 kwa wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu uliotolewa kwa kikundi cha Vijana cha Lordfather amesema kwamba hatua hiyo ni moja ya jitihada za serikali katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa ajira.

‎Katibu wa kampuni, Kassim Mgambo, naye amewashauri vijana kuacha kuishi kwa matarajio ya kuajiriwa na badala yake kuwekeza kwenye fursa zinazowazunguka.

‎“Mafanikio haya yametokana na kuanza na kidogo tulichokuwa nacho. Vijana wenzangu, anzisheni kitu hata kama ni kidogo lakini kianzeni kwa bidii na uaminifu. Serikali na wadau wanasaidia wale wanaothubutu,” amesema Mgambo.

Katibu wa Kampuni ya Lord father, Kassim Mgambo akiendelea na kazi ya usindikaji wa mvinyo katika kiwanda cha Lordfather kilichopo Kitwiru halmashauri ya Manispaa ya Iringa. Picha na Christina Thobias

‎Maoni ya wananchi na vijana wengine

‎Rehema Mgaya, mfanyabiashara wa Iringa mjini, amesema mradi huo umetoa hamasa kubwa kwa jamii.

‎“Siku hizi vijana wengi wameanza kujiuliza kama Lord Father wameweza, kwanini sisi tushindwe? Huu ni mfano mzuri,” amesema Rehema

‎Vijana wengine wa Iringa pia wameuona mradi huo kama fursa ya kujifunza.

‎Peter Nyagawa, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho Chuo Kikuu cha Iringa, amesema.

‎“Nimejifunza kuwa mafunzo tunayopata darasani yanaweza kutuletea kipato,” amesema

‎Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamehimiza serikali kutoa elimu zaidi kuhusu ujasiriamali na mikopo.

‎“Kuna vijana wengi wenye mawazo, lakini hawajui pa kuanzia. Kama tungekuwa na mafunzo ya mara kwa mara, miradi kama hii ingeongezeka,” amesema John Kipacha, mkazi wa Kihesa halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

‎Akizungumzia changamoto zinazokabili mradi huo, Mgambo amesema wanaendelea kukabiliana ukosefu wa eneo kubwa kwa ajili ya kiwanda cha kisasa na ufinyu wa mtaji wa kununua vifaa vya kisasa vya uzalishaji.

‎Pia, uhitaji wa kupanua masoko na kuwa na mawakala wa kudumu katika mikoa mingine ni jambo linalohitaji uwekezaji zaidi.

Mikakati ya baadaye ya kiwanda

‎Mgambo amesisitiza kuwa kampuni inalenga kufikia thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 katika kipindi cha miaka mitano ijayo na kuwa mmoja wa wazalishaji wakuu wa mvinyo Afrika Mashariki huku pia, ikipanga kuongeza aina za bidhaa na kuingia kwenye masoko ya kimataifa.