VYAMA 17 VYAREJESHA FOMU ZA KUTEULIWA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KIGAMBONI

 Na Mwandishi Wetu.

VYAMA 17 vyama vilivyochukua fomu za kuteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Kigamboni vimerejesha fomu hizo na tayari zimebandikwa ili ziweze kukaguliwa na kama kutakuwa na upungufu wagombea wanaweza kuwekewa pingamizi.

Aidha, wagombea wote wameteuliwa kugombea nafasi hiyo kwa hatua ya kuanza kampeni, kama hakutakuwa na pingamizi kwa wagombea yeyote katika jimbo hilo.

Hayo yamesemwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigamboni, Selemani Kateti  jijini Dar es Salaam kwamba vyama vyote  17 vilivyochukua fomu za kuteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge, vimerejesha fomu hizo na tayari zimebandikwa.

Kateti amesema hayo baada ya kufunga mchakato wa kumaliza kupokea fomu hizo na kuzibandika, vyama vilikuwa 18 vilivyochukua fomu ni 17 na vyote vimerudisha fomu hizo.

Amesema kuwa mchakato huo ulianza jana saa 1:30 asubuhi hadi saa 10 jioni na fomu zimezibandikwa kuanzia muda huo hadi leo saa 10 jioni, kama kutakuwa na pingamizi kwa wagombea watapokea kama utaratibu unavyoelekeza.

“Mchakato umekwenda vizuri wagombea wote wamerejesha fomu zao kuanzia saa moja asubuhi na hakuna malalamiko yoyote wala changamoto,”Amesema Kateti 

Kateti  amesema wahusika ambao ndiyo wenye mamlaka ya kuweka pingamizi ni Mgombea Ubunge wa jimbo husika, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Atakayeleta pingamizi dhidi ya mgombea yeyote atatakiwa kujaza fomu namba 9B kueleza pingamizi analoweka na kuliwasilisha kwa msimamizi wa uchunguzi kwa ajili ya hatua nyingine” Amesema Kateti 

Amesema zipo sababu 16 za mgombea kuwekewa pingamizi ikiwemo kama si raia wa Tanzania, kutiwa hatiani kwa kosa la kukwepa kulipa kodi na pia kama hajalipa dhamana ya Sh 50,000.

“Ikitokea mgombea yeyote amewekewa pingamizi anaweza kukata rufaa ndani ya muda uliyopangwa,”Amesema Kateti.

Msimamizi wa Uchunguzi Jimbo la Kigamboni, Selemani Kateti.