Wadau waonyesha njia kukabili tatizo la ajira

Arusha. Ufanisi mdogo wa vitendo katika utendaji kazi miongoni mwa wahitimu wa vyuo vikuu nchini, umeelezwa kuwa moja ya kikwazo cha vijana kushindana katika soko la ajira, ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo, Alhamisi Agosti 28, 2025, jijini Arusha na Mhadhiri na Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Evaristo Mtitu, wakati akizungumza katika kikao cha wadau wa elimu, kilichofanyika chini ya mradi wa kuimarisha uwezo wa taasisi za elimu ya juu nchini, unaolenga kuongeza uhusiano kati ya elimu na soko la ajira.

Mradi huo, unaofahamika kama China Fund In Trust Project Phase III (CFT-III), unatekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), kwa lengo la kuongeza uwezo wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini ili ziweze kukabiliana kikamilifu na mahitaji ya sasa ya ajira na maendeleo ya kiuchumi.

Dk Mtitu amesema kuwa changamoto kubwa inayojitokeza ni wahitimu wengi kushindwa kuendana na uhalisia wa soko la ajira, hasa kwa kushindwa kutumia maarifa yao kwa vitendo, jambo linalowapunguzia ushindani na fursa.

 “Wahitimu wengi wamefaulu vizuri, lakini inapokuja kwenye utendaji kazi, wanakosa ujuzi unaotakiwa ili waweze kuchangia kwenye uzalishaji katika maeneo ya ajira na hivyo kushindwa kupata ajira,” amesema Dk Mtitu.

Mdau wa elimu, Charles Ndahani, amesema mradi huu ulioanza utekelezaji katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), utasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, hasa kutokana na changamoto ya kushindwa kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Mkuu wa Kitengo cha Elimu kutoka Unesco, Dk Faith Shayo, amesema lengo la mradi huo ni kuongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu ili kukabiliana na mahitaji ya ujuzi kwa maendeleo ya Taifa.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Mariam Ismail, amesema kuwa suala la kufanya mapitio mara kwa mara ya mitaala ya elimu nchini limelenga kuendelea kuboresha sekta hiyo muhimu.

Amesema maboresho katika sekta hiyo yataendelea ili kuhakikisha kuwa mifumo inabadilika na wanafunzi wanatumia muda mdogo darasani na mwingi katika maeneo ya kazi, ili kujifunza mbinu mbalimbali.