Wagombea udiwani 16 CCM kupigiwa kura za ndiyo au hapana uchaguzi mkuu Kigoma

Kigoma. Wakati kampeni zikianza kote nchini katika nafasi za ubunge, udiwani na urais, Chama cha Mapinduzi (CCM)  mkoani Kigoma wagombea udiwani katika kata 16 wanatarajiwa kupigiwa kura za ndiyo au hapana baada ya vyama vya upinzani kutosimamisha wagombea katika kata hizo.

Mkoa wa Kigoma una jumla ya kata 139 ambapo kuelekea uchaguzi mkuu mwezi oktoba ni kata 123 pekee ndizo zenye wagombea kutoka vyama vingine vya siasa.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Agosti 28, 2025 katibu wa siasa, uenezi na mafunzo mkoani Kigoma Deogratius Nsokolo amesema wanaamini ushindi utakuwa kishindo, huku akiwashukuru wananchi katika kata hizo kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa kwa kuthamini maendeleo yaliyoletwa na Serikali.

‘’Hatuna shaka kwamba kuwepo kwa wagombea pekee katika kata hizo maana yake ni ukubalifu wa CCM mpaka wenzetu wanaona kwamba katika maeneo hayo wasiwe na wagombea ni ishara kwamba CCM inakubalika katika kata zote 139’’ amesema Nsokolo.

Amezitaja kata ambazo wagombea wake hawana upinzani kuwa kama inavyoonekana idadi katika mabano Wilaya ya Kasulu (6) ni Herushingo, Makere, Shunguliba, Kurugongo, Murufiti na Ruhita, wilayani Uvinza (1) kata ya Basanza, Kibondo (4) ambazo ni kata ya Mabamba, Bunyambo, Rugongwe na Mkabuye na wilayani Buhigwe kata (5) ambazo ni Mkatanga, Mwayaya, Munzeze, Mubanga na kata ya Kilelema.

Kuhusu wagombea ubunge hususan Jimbo la Kigoma mjini Nsokolo amesema kuwa chama hicho kimejipanga kumstaafisha siasa mgombea wa ACT Wazalendo ambaye aliwahi kuongoza jimbo hilo 2015-2025.

‘’Tunaye mgombea wetu ambaye anakwenda kumsukuma nje yule jamaa ambaye tangu tumemteua Baba Levo, wamepoteana na tutamstaafisha,’’ amesema.

Baadhi ya wagombea ubunge waliohudhuria katika hafla ya ufunguzi wa kampeni wamesema kuwa wamejipanga kupiga kampeni kunadi ilani ya chama hicho nyumba kwa nyumba.

Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Kasulu Mjini, amesema kuwa wananchi wake watarajie kampeni za furaha na kuwa hata wakati utakapofika wa kupiga kura waende kwa furaha kwa kuwa CCM chama chake kitashinda.

Naye Profesa Pius Yanda mgombea katika Jimbo la Buhigwe amesema kupitia uzoefu alionao kupitia tafiti nyingi alizozifanya akiwa mhadhili na huku akishiriki kuandaa Dira ya 2050 akishinda atakwenda kutekeleza aliyofanyia utafiti kwa muda mrefu.

‘’Mimi nimekuwa mtafiti kwa muda mrefu na nimehusika kuandaa Dira ya 2050 kwa hiyo nimeshawishika kuyaweka katika vitendo hasa uhitaji wa miundombinu ya Barabara kusafirisha zao la tangawizi ndiyo kipaumbele zaidi,‘’ amesema Profesa Yanda.