Wasafirishaji abiria wafurahia neema ya kampeni za CCM

Dar es Salaam. Ufunguzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) unaofanyika leo Alhamisi Agosti 28, 2025 katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, umegeuka fursa ya kiuchumi kwa wasafirishaji wa abiria wa ndani.

Madereva wa daladala, bodaboda na bajaj wameelezea kufurahia neema ya kipato baada ya vyombo vyao vya usafiri kukodiwa kwa wingi kupeleka wananchi kwenye mkutano huo.

New Content Item (1)

Wanachama kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wanahitaji usafiri wa haraka na wa uhakika kufika Kawe, hali inayosababisha ongezeko kubwa la wateja kwa wasafirishaji hao ukilinganisha na siku za kawaida.

Baadhi ya mabasi yanayotumika kusafirisha abiria kwa siku ya leo, mengi yamekodishwa na makundi ya watu kwa ajili ya kuwapeleka moja kwa moja kwenye viwanja hivyo.

Ili kurahisisha utaratibu wa kuondoka jioni, daladala na magari ya kukodi (special hire) yameandikwa majina ya vituo na maeneo ya asili yalipotoka, hatua iliyosaidia kupunguza usumbufu.

Akizungumza na Mwananchi, Abas Kambuga, kondakta wa daladala inayofanya safari zake kati ya Buyuni, Chanika hadi Simu 2000, amesema uzinduzi wa kampeni za CCM leo zitamsaidia kufunga hesabu zake mapema.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Hii leo nimepunguza kazi ya kupiga kelele kutafuta abiria. Tumekodiwa kupeleka wanachama Kawe kwa Sh120,000 kwenda na kurudi. Wameshalipa, kwa hiyo kazi imekuwa rahisi na tumepata kipato kizuri kwa siku moja,” amesema Kambuga.

Kwa upande wake, Ramadhan Rajab, kondakta wa basi linalosafairisha abiria kati ya Morogoro na Dar es Salaam, amesema alikodiwa na kundi la wanachama kutoka eneo la Kwa Mathias, Mkoa wa Pwani, kwa Sh500,000 kwenda na kurudi.
“Nilipigiwa simu usiku nikiwa Morogoro nijiandae kuwasafirisha. Safari kama hizi za mikutano ya kisiasa zinakuwa fursa ya mapato mazuri kwetu, kwa sababu malipo huwa makubwa na tunafunga hesabu mapema,” amesema Rajab.

Dereva wa bajaj, Mussa Mussa, amesema naye alinufaika baada ya kukodiwa na kikundi cha akinamama kutoka Magomeni waliotaka usafiri wa moja kwa moja bila kusimama.
“Wametulipa zaidi ya nauli ya kawaida, jambo lililotusaidia kupata kipato cha haraka na cha kutosha. Wengi wetu tumeona neema kupitia tukio hili,” amesema.

Naye Hassan Amir, bodaboda wa eneo la Mwenge, amesema: “Nilifanya safari nne mfululizo kutoka Mwenge hadi Kawe. Kwa siku ya kawaida si rahisi kupata mzigo kama huo, ila leo tumebahatika sana.”

Aidha, baadhi ya wamiliki wa magari binafsi nao wamejipatia kipato baada ya kukodiwa na makundi ya wanachama waliotaka kwenda pamoja kwa urahisi zaidi.

Katika kituo cha daladala kilichopo karibu na viwanja vya Tanganyika Packers, magari yamepewa utaratibu maalumu wa kuingia na kushusha abiria viwanja vya Kawe.

Baada ya kushusha abiria, magari mengine yameendelea na ratiba za kawaida huku sehemu nyingine zikiwekwa kwa maegesho ya muda.

Tito Kisoa, kondakta wa daladala ya Mbezi–Mbagala, amesema wameondoka baada ya kushusha abiria kutokana na makubaliano ya awali.
“Wangesema tubaki tungesubiri, lakini kwa malipo tuliyopokea tulipaswa kuendelea na ratiba nyingine. Bosi anasubiri hesabu na sisi pia tunahitaji kipato chetu,” amesema.