Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema wingi wa watu waliojitokeza katika uwanja huo unadhihirisha kuwa CCM ina uwezekano wa kuendelea kukamata dola.
“Sasa nawauliza wanaotaka dola kutoka kwetu wataipata? Wataweza? Wataweza kweli… lakini hatuwezi kuongelea wenyewe lazima tupate watu wa kutusindikiza, kwa hiyo tunawakaribisha wasindikizaji wetu lakini tunawaambia tumejiandaa kwa kiwango kikubwa katika kuendelea kukamata Dola,” amesema.
Amesema CCM lengo lake ni ustawi wa Watanzania wote na wanaamini katika utu, usawa na kujitegemea kwa Taifa na ndiyo vitu wanavyosimamia.
Amesema Samia ana historia ndefu katika uongozi wa nchi, alianza kufanya kazi katika jamii baadaye akaingia baraza la uwakilishi Zanzibar kabla kuhamia baraza la Mawaziri la Muungano.
Amesema mwaka 2015 kulikuwa na uchaguzi mkuu na aliyeteuliwa kuwa mgombea urais hayati John Magufuli alimteua Samia Suluhu Hassan kuwa makamu wake.
Uteuzi huo ulimwezesha kutembea Tanzania nzima na kuifahamu Tanzania na alihudumu kwa miaka mitano kama Makamu wa Rais hivyo anaijua nchi, chama na Serikali.
Amesema mwaka 2020 uchaguzi ulifanyika na hayati Magufuli hakupingwa kama ilivyo kanuni ya chama ndipo alimchagua Samia kuwa msaidizi wake kwa mara ya pili.
“Ninapokuja kumtambulisha namtambulisha mtu mnayemjua vizuri,” amesema Wasira.
Amesema kwa sababu ya matatizo ya mfumo dume wengine walifikiri usipokuwa mwanaume hauwi rais, wengine walikuwa rafiki wa marehemu (hayati Magufuli), ni haki yao walikuwa na hofu mabadiliko yale wakijiuliza yatawaacha wapi.
“Walitofautisha matakwa yao na ya Watanzania, matatizo tunayosikia nje huko yanatokana na hofu hiyo ya kawaida tu, hofu ilikiwa kubwa kwa sababu kulikuwa na miradi mikubwa na Watanzania wengine waliamini isingekuwa rahisi kwa Samia kuitekeleza, lakini matokeo yake Samia kwa kutumia kauli mbiu ya maneno mawili alisema kazi iendelee,” amesema Wasira.
Amesema matokeo yake kazi imeendelea na hofu zilizokiwapo hazimo ndiyo maana tunatambua kuwa jamii ina makundi mengi aliyatembelea ikiwemo viongozi wa dini, wahariri wa vyombo vya habari waliokuwa wakidai haki ya vyombo vya habari imeminywa na walipewa uhuru wa kukosoa kwa haki ili isaidie kujua wapi ambapo hawaendi vizuri kama Serikali.
Pia vyama vya siasa vilivyokuwa vikinung’unika vilikutana naye na kukubali mambo mengi aliyoshauriwa kupitia kamati maalumu ya vyama hivyo.
“Samia hakuingia kwa urahisi, aliachiwa kazi na miradi mikubwa na watu wakawa na mashaka kama itatekelezwa,” amesema.
Amesema Samia ameendeleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo reli ya kisasa inayosubiriwa kwa hamu na wakazi wa Kigoma, Mwanza na Tabora.
“Tumpe mitano tena akamalizie kazi aliyokuwa ameanza. Katika elimu pia amejenga shule nyingi, hospitali, vituo vya afya. Huyo ndiyo Samia Suluhu Hassan tunayemleta kwenu,” amesema.