Wataja mbinu kuboresha elimu watu ya  wazima

Dar es Salaam. Wataalamu mbalimbali wa elimu nchini wametoa mapendekezo manne ya kuboresha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania (TEWW).

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na Serikali kuandaa waraka utakaowasaidia wanafunzi wanaotoka nje ya mfumo rasmi wa elimu, kurudi kwenye masomo kupitia taasisi hiyo kwa lazima.

Pia, wamependekeza Serikali kuandaa waraka wa elimu utakaoelekeza kila kata iwe na vituo vya elimu jumuishi ili elimu inayotolewa kwa watu wazima iwe rafiki.

Akizungumza leo Alhamisi Agosti 28, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga  maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW, Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Philipo Sanga amesema wataalamu wamependekeza uwepo wa waraka huo utakaosaidia kuwafanya wanafunzi wanaotoka nje ya mfumo wa elimu kurudi kwa lazima kupitia mfumo usio rasmi.

“Tumependekeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iandae waraka utakaoelekeza kila kata iwe na kituo jumuishi. Tunataka kila kata iongeze fursa ya watu kujipatia elimu,” amesema.

Pendekezo la tatu, Profesa huyo ametaja, ni kupitia upya mwongozo wa elimu ya watu wazima ili kuufanya uendane na mazingira ya sasa.

“Lengo la kupitia mwongozo huo ni kuufanya utoe tafsiri sahihi ya wajumbe katika mikutano husika na kuwapatia majukumu yao. Kukosekana kwa utashi wa kisiasa kumesababisha kusuasua kwa mwongozo huo,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi Idara ya Elimu Atupele Mwambene

Pendekezo la nne, Profesa Sanga ametaja ni kuundwa kwa kada za elimu ya watu wazima kuanzia ngazi ya halmashauri hadi Taifa ili kuchochea ufanisi wa utendaji katika taasisi hiyo.

Akifunga maadhimisho hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali itailinda taasisi hiyo na ameahidi kufanyika kwa  mapitio makubwa ya sheria iliyounda taasisi hiyo ili kuifanya idumu zaidi.

“Tunajipanga kufungua ukurasa mpya kwa mapendekezo haya mliyoyasema, na haya yamewezekana kwa sababu tunao wadau,” amesema.

Amesema Serikali itahakikisha jukumu la taasisi hiyo linafahamika kwa ufasaha na kuondoa mkanganyiko uliopo dhidi ya taasisi hiyo na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), pamoja na kufuta dhana ya watu kusema taasisi hiyo haihitajiki.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Idara ya Elimu, Atupele Mwambene amesema kongamano hilo ni sehemu muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema mafanikio katika mpango wa elimu nje ya mfumo rasmi wa elimu ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya 2050 inayolenga kuwapo kwa Watanzania wenye ujuzi.