……………..
Na Sixmund Begashe, Dodoma
Wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maliasili na Utalii wametakiwa kuzingatia matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi katika uchakataji, uhifadhi na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara hiyo, Bi. Bure Nassibu, alipokuwa akifunga kikao kazi cha siku mbili kilicholenga kujadili na kupanga mikakati ya utekelezaji wa shughuli za ufuatiliaji na Tathmini ya Sera, Mipango, Mpango Mkakati na Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030.
Amesema pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali, watumishi hao wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu huku wakizingatia kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma kwa kuwa Wizara inawategemea katika kusukuma mbele mafanikio ya utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha, amewasisitizia kushirikiana kikamilifu na viongozi pamoja na watumishi wa idara, vitengo na taasisi zao ili kuimarisha uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa Ufuatiliaji na Tathmini katika majukumu ya kila siku.