Dar es Salaam. Shauri la utata wa uteuzi wa mgombea urais wa chama cha ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 limetajwa mahakamani kwa mara ya kwanza, huku Mahakama ikisema haitasita kusimamia haki itakaporidhika kuhusu uwepo wa ukiukwaji wa taratibu.
Shauri hilo limefunguliwa jana, Agosti 27, 2025, Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma, na Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa ACT-Wazalendo na mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Luhaga Mpina, dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa Mpina kuomba kuteuliwa na INEC kuwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, na wa INEC kumzuia kurejesha fomu ya kuomba uteuzi aliyokabidhiwa awali na tume.
Katika shauri hilo namba 21692 la mwaka 2025, lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, waombaji, pamoja na mambo mengine, wameiomba Mahakama iielekeze INEC ipokee fomu ya mgombea huyo kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.
Shauri hilo linalosikilizwa na majaji— Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza limetajwa mahakamani hapo leo, Agosti 28, kwa mara ya kwanza.
Waombaji wamewakilishwa na jopo la mawakili John Seka, Edson Kilatu, John Madeleka, Mwanaisha Mdeme na Jaspar Sabuni, huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method, akishirikiana na mawakili wa Serikali, Stanley Kalokola na Erigh Rumisha.
Mbali na nafuu zinazoombwa, pia wameomba Mahakama iiamuru INEC isimamishe kwa muda mchakato wa uteuzi wa wagombea wa urais kusubiri shauri hilo kusikilizwa likishirikisha pande zote.
Mahakama, katika amri zilizotolewa na Jaji Kagomba, imekataa maombi ya kusimamisha mchakato wa uteuzi wa wagombea urais ambao uko katika hatua ya pingamizi inayohitimishwa leo (Agosti 28), ikisema mchakato wa uteuzi umeshakamilika tangu jana (Agosti 27).
Hata hivyo, Jaji Kagomba amesema Mahakama ina wajibu wa kuangalia yote yaliyofanyika kama yamezingatia sheria na Katiba na kwamba, ikijiridhisha kuwa taratibu za kisheria na kikatiba hazikufuatwa katika kuondolewa kwa mwombaji wa pili (Mpina), haitasita kutoa amri zitakazomrudishia haki zake.
Wajibu maombi wameomba wapewe siku 14 kuwasilisha maelezo ya utetezi wa maandishi na kiapo kinzani, kwa mujibu wa sheria.
Mawakili wa waombaji walipinga ombi hilo, wakidai kesi imefunguliwa chini ya hati ya dharura, huku wakiomba wajibu maombi wapewe muda mfupi zaidi, ikiwezekana siku moja.
Mahakama imewapa wajibu maombi siku tano wawe wamewasilisha majibu na kiapo kinzani mpaka Septemba 2, 2025, huku ikipanga Septemba 3 kuwa siku ya kutajwa kesi hiyo.
Mbali na hayo, Mahakama imesema kwa kuwa kesi hiyo ina masilahi ya umma, ingawa itaendeshwa kwa mtandao, wananchi wanaruhusiwa kujiunga kupitia kiungo kitakachotolewa.
Pia imetoa wito kwa wananchi kutambua kuwa watakuwa mahakamani, hivyo wanapaswa wazingatie nidhamu ya uendeshaji mashauri mahakamani, hawapaswi kurekodi.
Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025, kuomba uteuzi wa INEC kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Hata hivyo, uteuzi wake umebatilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na pingamizi lililowasilishwa kwake na Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala.
Alidai uteuzi huo ni batili kwa kuwa Mpina hana sifa kutokana na kutokutimiza vigezo vya kikanuni, akirejea Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa Chama, Toleo la mwaka 2015, kanuni namba 16(4) (i-iv).
Akirejea kanuni hizo, Monalisa alibainisha kuwa kanuni ya 16(4)(i) inaeleza mgombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa, anapaswa awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.
Kanuni ya 16(4)(iii) anapaswa awe tayari kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kabla ya kuteuliwa kugombea, kwa kufuata utaratibu ulioainishwa katika sehemu ya VI ya nyongeza ya Katiba ya ACT-Wazalendo.
Kanuni ya 16(4)(iv) anapaswa awe ni mtu aliyethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aoneshe utayari wa kuisimamia na kuiishi.
Monalisa alibainisha kuwa Mpina anakosa sifa zote hizo, kwa kuwa alijiunga na chama hicho Agosti 5, 2025, na alipitishwa na mkutano mkuu kuwa mgombea wa chama hicho Agosti 6, siku moja baada ya kujiunga na chama hicho.
Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya kusikiliza pande zote alikubaliana na hoja za pingamizi la Monalisa na kutengua uteuzi wa Mpina.
Kutokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, INEC ilimuondoa Mpina katika orodha ya walioomba kuteuliwa kugombea urais katika uchaguzi huo na kumzuia asijitokeze siku ya uteuzi.
Hata hivyo, Mpina na ujumbe wake jana, Agosti 27, alikwenda ofisi za INEC jijini Dodoma kwa lengo la kurejesha fomu kuomba kuteuliwa, lakini alizuiwa na maofisa wa polisi kuingia ndani ya ofisi hizo.