Aondolewa uvimbe wa kilo mbili kwenye pafu Hospitali ya KCMC

Moshi. Jopo la madaktari bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) limefanikiwa kuondoa uvimbe mkubwa wenye uzito wa kilo mbili kwenye pafu la kushoto la kijana mwenye umri wa miaka 30, ambaye alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kupumua kwa muda mrefu.

Upasuaji huo unaofahamika kitaalamu kama Thoracotomy with Tumor Excision (upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye kifua) ulifanyika  Agosti 28, 2025  na kuchukua muda wa saa tano chini ya madaktari bingwa wa hospitali hiyo, Profesa Kondo Chilonga, kwa kushirikiana na Daktari Hiten Solanki na timu ya wataalamu wengine.

Akizungumza kuhusu upasuaji huo, Dk Hiten Solanki amesema mgonjwa huyo alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kupumua kwa muda mrefu kabla ya kufikishwa hospitali ya KCMC kwa uchunguzi zaidi.

“Baada ya kufanyiwa vipimo mbalimbali vya CT Scan ya kifua, tuligundua kuwepo kwa uvimbe mkubwa kwenye pafu la kushoto pamoja na maji mengi kwenye mapafu,  tulikaa kama jopo la madaktari bingwa tukamfanyia upasuaji ambao ulifanikiwa kuondoa uvimbe wa kilo mbili,” amesema  Dk Solanki.

Aidha, Dk Solanki amesema  kuwa mgonjwa huyo kwa sasa yupo chini ya uangalizi wa karibu wa wataalamu na anaendelea na matibabu akiwa katika hali ya kuridhisha.

Aidha, amewataka Watanzania kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili magonjwa yanapobainika  mapema yaweze  kutibiwa kabla hayajawa sugu au hatarishi kwa maisha.

Ofisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo amesema mgonjwa huyo anaendelea vizuri baada ya upasuaji na muda si mrefu anatarajiwa kuhamishwa kutoka chumba cha uangalizi maalumu (ICU) na kupelekwa wodi ya kawaida.

“Tunaishukuru timu ya madaktari wetu bingwa kwa mafanikio haya makubwa, . Mgonjwa alipelekwa ICU baada ya upasuaji, na sasa anaendelea vizuri,” amesema Chisseo

Amesema, “Tunamshukuru Mungu leo mgonjwa anaendelea vizuri na baada ya siku mbili atapelekwa kwenye wodi za kawaida, kwa sasa ana uwezo wa kuongea na kwa sababu za taratibu za kimatibabu harusiwi kuongea ataongea wakati akishatoka ICU.”