Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amewataka wagombea wote wa nafasi za udiwani na ubunge kupitia chama hicho kuwafikia wananchi katika kipindi hiki cha kampeni na kuwaeleza kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25, pamoja na mipango na sera za chama kuelekea mwaka 2030.
Aidha, katika hotuba yake, Rais Samia mbali na kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake pamoja na vipaumbele vya sasa, aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni ya wagombea wa CCM ili kupata fursa ya kusikiliza sera na mipango ya chama.
Alisisitiza kuwa kufanya hivyo kutawaweka wananchi katika nafasi nzuri ya kufanya maamuzi sahihi ya kuwachagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo katika miaka mitano ijayo.
Akizungumza, Agosti 28, 2025, mbele ya umati wa wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za kitaifa za CCM, Rais Samia – akiambatana na mgombea mwenza wake, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi – aliwashukuru wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na mikoa jirani kwa kujitokeza kwa wingi.
Alisema nguvu ya CCM imejengwa katika misingi ya umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.


Related