CHAN 2024: Sudan, Senegal ushindi lazima

WABABE wawili kutoka kundi moja D, Senegal na Sudan wanakutana tena leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Mandela, jijini Kampala, Uganda kutafuta mshindi wa tatu katika mashindano ya ubingwa wa mataifa ya Afrika (CHAN) 2024.

Timu hizi zilikutana Agosti 19 katika mechi ya mwisho ya makundi visiwani Zanzibar, ambapo hakupatikana mbabe, lakini leo ni lazima mshindi apatikane hata kama ni kwa matuta, tofauti na pambano lile la awali ambalo lilizivusha zote kutinga robo fainali kila moja ikifikisha pointi tano.

Katika hatua ya robo fainali, Sudan iliing’oa Algeria kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kutoka sare (1-1) ndani ya dakika 120, Senegal waliokuwa wakitaka kutetea taji kwa msimu wa pili mfululizo waliitoa Uganda kwa kuichapa bao 1-0.

Sudan ilikwamia kwa Madagascar katika nusu fainali kwa kufungwa bao 1-0 ndani ya dakika 120, huku Senegal ilivuliwa taji na Morocco kwa penalti 5-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120.

Hii itakuwa mara ya sita kwa Senegal na Sudan kukutana kwa miaka ya hivi karibuni katika mashindano yote ikiwamo mechi za kirafiki, huu ni mechi moja tu kati ya hizo ambayo imetoa zaidi ya mabao matatu.

Vijana wa James Kwesi Appiah watakuwa kwenye mtego wa kusaka ushindi wa kwanza dhidi ya Senegal kwani katika mechi tano ambazo wamekutana, wamefungwa tatu na mbili wametoa sare mfululizo.

Mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana ni Januari 12,2012 na Senegal iliifunga Sudan bao 1-0 kwenye mechi ya kirafiki, miaka sita baadaye, 2018 walikutana tena katika mechi mbili za kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika.

Katika mechi ya kwanza, Senegal ilishinda kwa mabao 3-0 na nyingine ikiwa ugenini ilishinda kwa bao 1-0. Walikutana tena, Machi 22 mwaka huu katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia wakatoka suluhu.