Dabi ya pili Kariakoo kabla ya Krismasi

WAKATI ukiendelea kutafakari ratiba ya mchezo wa ufunguzi wa ligi Ngao ya Jamii kati ya watani wa jadi Simba na Yanga, Dabi ya Kariakoo iliyopigwa kuchezwa Septemba 16 timu hizo mbili zitakutana tena Desemba 13, mwaka huu kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo utakuwa wa duru ya kwanza kwa wawili hao ambapo Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba na katika ratiba ya awali iliyotolewa leo Agosti 29, 2025 Bodi ya Ligi (TPLB) imetangaza rasmi ligi itaanza Septemba 17 kwa mechi mbili za ufunguzi.

Ratiba hiyo inaonyesha Ligi Kuu itaanza Septemba 17 kwa michezo miwili kati ya KMC na Dodoma Jiji – mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam na mchezo mwingine utakuwa kati ya Coastal Union dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani – Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Ibrahim Mwayela amesema upangaji wa ratiba hiyo umezingatia mashindano yote ya ndani na nje ikiwa ni pamoja na mashindano ya CHAN 2025 ambayo Tanzania ni nchi mwenyeji.

“Tunatambua tuna ratiba ngumu kutokana na uwepo wa michuano mingi hivi karibuni lakini katika kuhakikisha tunakuwa na ratiba imara tumezingatia mashindano yote,” amesema na kuongeza:

“Tunatarajia kumaliza ligi Mei 23 kama ratiba ilivyopangwa. Hakutakuwa na sababu ya mchezo wowote kuahirishwa hii ni kutokana na namna ambavyo ratiba imepangwa kwa kuzingatia mashindano yote.”

Amesema wanatambua ratiba itakuwa inabana lakini katika kuhakikisha ligi inaisha mapema wamezingatia muda wa kikanuni kupanga ratiba kwa kuzingatia mechi zote kuanzia wawakilishi wa kimataifa Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars.

“Ukiondoa wawakilishi hao pia tumezingatia timu kutoka kituo kimoja kwenda kingine kwa kuangalia kanuni na muda wa Shirikisho la Soka duniani. Hatutarajii malalamiko kutoka kwa klabu,” amesema.