Shinyanga. Wanafunzi wa Shule ya Msingi Shingida Kata ya Usanda, Wilaya ya Shinyanga wanakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo, ambapo yaliyopo hivi sasa ni matatu na yanatumiwa na wanafunzi zaidi ya 1000 (wastani wa wanafunzi 330 kwa tundu moja).
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Singita Fransisico Machungwa leo Agosti 29, 2025 wakati akieleza changamoto zilizopo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro alipokuwa akipokea kero za wananchi ili kuchukuwa hatua.
Amesema matundu manane ya vyoo katika shule ya msingi Shingita yametitia na kubaki matundu matatu ambayo yanatumika moja kwa wasichana na mawili wavulana hali ambayo inahatarisha afya za wanafunzi kutokana na kuwa na msongamano wa wanafunzi.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya tuna changamoto ya matundu ya vyoo shule ya msingi Shingida yenye wanafunzi zaidi ya 1,000 matundu yanayotumika ni matatu tunahofia inaweza kufungwa muda wowote tunaomba utusaidie fedha itoke tuanze ujenzi,” amesema Mwenyekiti Machungwa.
Amesema halmashauri ya kijiji inazaidi ya Sh28 milioni ambazo ni fedha walizokusanya kutokana na ushuru wa minara iliyopo katika kijiji hicho, lakini wameshindwa kutoa fedha hizo kutokana na taratibu za mifumo ya fedha jambo ambalo linakwamisha kuanza kazi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga Mwita Warioba amesema atamuagiza afisa manunuzi kushughulikia suala hilo ili ujenzi uanze.
Kufuatia changamoto hiyo, Mkuu wa Wilaya, Mtatiro ametoa wiki moja kwa uongozi wa Halmashauri kukamilisha zoezi la utoaji wa fedha zinazo kusanywa kutoka kwenye ushuru wa minara ya mlima Kilulu ili ujenzi uanze mara moja.
Amesema wiki ijayo atafika katika shule hiyo kushirikiana na wananchi kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo Shule hiyo ili kuwawezesha wanafunzi kuwa katika mazingira mazuri.