Mwanza. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameeleza jinsi chama hicho kitawafanyia wananchi wa mkoa wa Mwanza endapo watapewa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Sekta ya elimu, afya, miundombinu ya barabara, huduma za maji na kijamii itakuwa ni kipaumbele kikubwa. Kuwasimamia na kuwawajibisha wabadhirifu wa mali za umma ni miongoni mwa mambo ambayo Serikali itakayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itayasimamia.
Dk Nchimbi ameyasema hayo leo Ijumaa, Agosti 29, 2025 katika mikutano ya kampeni ya uchaguzi mkuu iliyofanyika wilaya ya Kwimba na Nyamagana mkoani Mwanza. Mikutano hiyo imetumika kuwanadi wagombea udiwani na ubunge.

Katika mikutano hiyo, Dk Nchimbi ameeleza yale ambayo Serikali ya CCM imeyafanya miaka minne ya Rais Samia akiwa madarakani na yale watakayoyafanya endapo watapewa ridhaa kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021 akichukua nafasi ya John Magufuli ambaye alifariki dunia Machi 17, 2021 baada ya kuumwa moyo.
Awali, Samia alikuwa makamu wa Rais. Samia akawa mwanamke wa kwanza kuwa Rais. Waliotangulia kwenye nafasi hiyo ni Julius Nyerere (1961-1985, Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Benjamin Mkapa (1995-2005), Jakaya Kikwete (2005-2015) na John Magufuli (2015-2021).
Akiwa Kwimba, Dk Nchimbi amesema:”Tunakuja tena kuwaomba mtuchague kwa sababu tumefanya mengi zaidi ya kiwango. Ilani yetu chini ya Mama Samia imetekelezwa na kila mmoja ameona.”
“Kutokana na kazi kubwa ambayo tumeifanya, ndiyo maana zaidi ya wagombea wetu 91 wa udiwani wa Mwanza wamepita bila kupigwa,” amesema Dk Nchimbi.
Aliposimama Buhongwa, wilayani Nyamagana kusalimia akitokea Kwimba amesema, watu wa Mwanza ukifanya vibaya watakupinga, ukifanya vizuri watakupongeza:”Na hili la madiwani wetu kupita bila kupingwa na chama chochote ni ishara tumefanya mazuri na mkitupa tena ridhaa niseme Mama Samia na mimi (Dk Nchimbi) yajayo yanafurahisha.”
Huku akishangiliwa, Dk Nchimbi aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM amesema:”Kasi ya miaka minne mmeiona, itakuwa mara dufu katika kuleta na kusimamia miradi ya maendeleo.”
Akiwaeleza mamia ya wananchi wa Kwimba, Dk Nchimbi amesema katika kipindi cha miaka minne, Hospitali mpya imejengwa Kwimba, vituo vya afya kutoka 50 hadi 61 na hii ni katika kuzingatia afya za wananchi wetu. Watumishi wa afya walikuwa 335 sasa wapo 513 kwa wilaya hiyo pekee.
Amesema shule za sekondari zimejengwa kutoka 34 hadi 41. Madarasa mapya yameongezeka kutoka 438 hadi 709, maji safi yameongezeka kutoka asilimia 36 hadi 77: “Yaani kila Wanakwimba 100, wanaopata majisafi 77. Vijiji vyenye umeme vimeongezeka kutoka 60 hadi 119. Ukisema CCM haijafanya kitu huyu atakuwa na lake jambo”
Dk Nchimbi amesema: “Yapo mambo mengi sana yamefanyika, viongozi wetu wa ngazi mbalimbali watayazungumza kwani tumeyafanya pamoja.”
Katika miaka mitano ijayo, Dk Nchimbi amesema watajenga zahanati mpya 20, ukiamka tu unaumwa, ukitoka nje ukitizama tu unaiona. Ujenzi wa zahanati nne ambazo ziko kwenye hatua mbalimbali ili ziwe zahanati 44.
Ameahidi kujenga vituo vipya vitano vya afya na kituo cha afya kinakaribiana na hospitali ya wilaya. Aidha, hospitali ya wilaya wanakusudia kuiimarisha zaidi kwenye huduma za kibingwa ziweze kupatikana.
Amesema jana Alhamisi kwenye uzinduzi wa kampeni uliofanywa na Rais Samia aliahidi ndani ya siku 100,
moja ya mambo ni kupata bima ya afya kwa wote, lakini wazee, watoto, wenye ulemavu na kina mama wajawazito utekelezaji wake utaanza ndani ya kipindi hicho.
Pia, ameahidi koongeza zaidi madarasa, walimu na mitaala, tunataka watoto wetu kuelimishwa na tunataka watoto wakaelimishwe sio kukua. Mtoto akiwa darasa la kwanza hadi tatu wawe na uwezo wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Kwenye huduma za maji, Dk Nchimbi amesema wataongeza upatikaji wa maji ili kila Wanakwimba 100, wanaopata maji safi iwe asilimia 90 na tunaweza kutekeleza zaidi.
Ujenzi wa barabara utazingatiwa kwa kiwango cha lami. Aidha, uboreshaji wa masoko itakuwa kipaumbele ili wakulima wanapolima wawe na uhakika wa mazoa yao kupata soko.
Tumewaletea wagombea wazuri
Awali, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge maarufu ‘smart’ amesema ukiwa katibu mkuu (Dk Nchimbi) ulifanya mambo mengi na kukifanya chama kuwa imara. Tunampongeza Dk Asha-Rose Migiro kushika kijiti.

Kuhusu maandalizi, amesema: “Sisi mkoa wa Mwanza tunaingia katika uchaguzi tukiwa kifua mbele kwani tuna mtaji wa kura kutoka kwa wanachama wetu waliojiandikisha zaidi ya laki saba na wengine wanaotuunga mkono.”
“Tumewaletea wagombea wazuri wa udiwani na ubunge tena vijana na tunawaomba tuendeleze umoja na amani: “Niwaombe wana CCM wenzangu, tufanye kampeni za kistaarabu na zenye tija.”
Endelea kufuatilia Mwananchi