*Asema atapiga marufuku hospitali zote nchini kuzuia miili ya marehemu inayodaiwa
*Kuanzisha gridi ya maji ya Taifa kwa ajili ya kuwa na vyanzo by uhakika vya maji
*Aahidi kuendeleza mashauriano na wadau kwa lengo la kufanikisha Katiba Mpya
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameeleza mambo kadhaa muhimu ambayo atayafanya katika kipindi cha siku 100 za mwanzo za uongozi wake baada ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu 2025.
Katika baadhi ya mambo atakayoanza nayo katika siku 100 za Serikali yake ni Serikali kutoa matibabu bure kwa wajawazito, wazee na Watoto kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote ambapo hiyo itakuwa ni hatua ya awali katika kutekeleza mpango wa Bima ya afya kwa wote kwa kuanza na makundi hayo.
Mengine atakayoanza nayo ni Serikali kupiga marufuku hospitali zote nchini kuzuia miili ya marehemu isichukukuliwe kwasababu ya kudaiwa fedha za matibabu na badala yake kutakuwa na utaratibu mzuri wa ndugu kuchukua mwili kwa ajili ya kwenda kuzika na kama kuna deni ndugu watalipa kwa utaratibu mzuri na sio kuzuia maiti.
Akizungumza na maelfu ya wananchi wa Dar es Salaam ambao walihudhuria uzinduzi wa kampeni rasmi za Chama hicho zilizofanyika Uwanja wa Tanganyika Peckers ,Rais Dk.Samia pamoja na mambo mengine ametaja vipaumbele vyake katika siku 100 za mwanzo baada ya kuunda Serikali.
Rais Samia Amefafanua kuwa kupitia Bima ya Afya kwa Wote, watazindua mfumo wa taifa kwa awamu ya majaribio kuanzia wazee, wototo, wajawazito ambapo gharama za matibabu zitabebwa kupitia mfuko wa bima ya afya.
Pia amesema serikali itagharamia kwa asilimia 100 wananchi wasiokuwa na uwezo kupata vipimo vya figo, moyo, sukari, mishipa ya fahamu na mifupa. “Tutatoa ajira 5000 katika sekta ya afya ndani ya siku 100 wakiwemo wauguzi na wakunga.
Akizungumza zaidi amesema katika siku 100 serikali yake itaweka mkakati wa elimu kisayansi ambao kila mtoto wa darasa la tatu atakuwa na uwezo wa kusoma, kuandika bila shida, sambamba na kuajiri walimu 7,000 wa masomo ya hisabati na sayansi.
Pia katika siku hizo 100 ,Serikali yake itatenga Sh.bilioni 200 ambazo zitawezesha kuwapatia mtaji wafanyabiashara wadogo na kati, uanzishwaji kampuni changa, kurasimisha wajasiriamali wadogo wakiwemo bodaboda, mama lishe, wafanyaviashara wadogo kuingizwa katika mfumo rasmi wa serikali.
Katika siku hizo 100 pia watazindua mpango wa Pamoja utakaohusisha waajiri, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, kulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele lengo likiwa ni kuwafanya wanafunzi wa VETA kuchukuliwa viwandani kufanyakazi zao za mazoezi.
Pia Serikali itaanzisha programu ya mitaa ya viwanda wilayani kwa lengo la kuzalisha ajira kupitia mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi madini na misitu na kuongeza serikali itakayoiunda itaanza ujenzi wa gridi ya taifa ya maji kwa lengo la kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji.
“Gridi hiyo itahusisha vyanzo vikuu vya maji ambavyo ni Ziwa Viktoria, Tanganyika, Nyasa na mito mikubwa.Pia tutaendelea kuendeleza jitihada nishati safi kupikia ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Rais Samia pia amesema ataweka mifumo rafiki ya uwajibikaji kwa mawaziri na wakuu wa mikoa kutakiwa kutoa taarifa na kujibu maswali kwa wananchi kwa njia ya simu.
Mengine atakayoanza nayo baada ya kuchaguliwa kuwa Rais ni kuendeleza mashauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi ikiwemo kuunda tume maalum kundaa mazingira ya mchakato wa katiba mpya.