SIMBA jana ilimtambulisha rasmi mshambuliaji mpya, Seleman Mwalimu ‘Gomes’ ambaye Mwanaspoti liliwataarifu mapema angetua Msimbazi kwa mkopo kutoka Wydad Casablanca ya Morocco, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids akiichambua kambi ya Misri.
Simba iliweka kambi ya karibu mwezi mzima nchini humo, ikianzia jiji la Ismailia kabla ya kuhamia Cairo na iliifunga rasmi juzi baada ya mechi dhidi ya FC Fassell, kisha kuanza safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kujiandaa na msimu mpya wa mashindano, huku Fadlu aliichambua kambi kuwa imempa manufaa makubwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema kwa kiasi kikubwa kambi hiyo imemsaidia kujenga muunganiko wa nyota wapya kikosini na amewaita mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Septemba 10 katika Tamasha la Simba Day wakiikaribisha Polisi Kenya akiahidi kuwa wamesuka kikosi bora cha ushindani.
Kocha amefunguka hayo baada ya timu yake kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya FC Fassell ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Liberia na timu kufunga kambi kwa mchezo huo huku nyota wote wakipata nafasi ya kucheza.
Fadlu alisema walikuwa na maandalizi mazuri na yenye tija kwa timu yao ambayo inajiandaa na michuano ya kimataifa Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi ya ndani huku akiweka wazi kuwa wamekipata kila kitu kilichowapeleka huko.
“Tumekuwa na maandalizi mazuri na yenye tija nimepata nafasi ya kuwapima wachezaji wangu wote faida kubwa niliyoipata ni wachezaji wapya kufanikiwa kuingia kwenye mbinu zangu haraka na kuongeza ushindani wa namba kikosini,” alisema Fadlu na kuongeza;
“Nafikiri kazi iliyobaki ni kuonyesha kwa vitendo kwenye mechi za ushindani nimefurahia maandalizi tuliyoyafanya. Tumefanikiwa kwa asilimia kubwa kwani matarajio yameenda vile tulivyopanga, tumecheza mechi za kirafiki za kutosha.”
Alitumia nafasi hiyo kuwaita mashabiki wake kujitokeza kwa wingi kushuhudia usajili wao walioufanya na viwango vya wachezaji wao ambao wameongeza nguvu kwenye maeneo ambayo yalikuwa na uhitaji msimu uliopita wakishindwa kutwaa taji la ndani.
“Mechi tulizocheza zilikuwa chachu ya kuunganisha wachezaji kuweza kuzoeana haraka ukizingatia kwa kiasi kikubwa timu tumeanza kuijenga upya kuwa na nyota wapya zaidi ya kumi kikosini kunahitaji muda wa kuwaunganisha,” alisema Fadlu na kuongeza;
“Nafurahi nafanya kazi na wachezaji wengi ambao tayari wana uzoefu, sijapata wakati mgumu kuwaunganisha na kufanya waweze kukopi mifumo yangu kwa uharaka, hii imenipa picha ya kuamini watafanya kazi bora kwenye mechi za ushindani zilizo mbele yetu.”
Simba tayari imerejea nchini na wikiendi hii inatarajia kufanya uzinduzi wa jezi zake za msimu kabla ya kuivaa Polisi Kenya ambayo ndio timu bingwa wa ligi nchini humo.
Ikiwa kambini Simba imecheza mechi nne za kirafiki ikiwamo ya Kahraba Ismailia waliyoifunga mabao 2-0, kisha kukumbana na kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa ENPPI ya Misri na kuifunga Wadi Deglas kwa mabao 2-0 kabla ya kufunga kambi na sare hiyo ya 1-1 na Waliberia.
Simba inarudi kujiandaa na Simba Day sambamba na mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Septemba 16 dhidi ya Yanga kabla ya kuifuata Gaborone United katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.