Dar es Salaam. Hekaheka za kusaka kura za nafasi ya urais katika wiki ya kwanza ya kampeni tayari zimeanza na kuvifanya vyama vya siasa kugawana maeneo ya nchi, kunadi sera zao kushawishi wananchi, ili wagombea wao wachaguliwe.
Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilichofungua pazia la kumnadi mgombea wake, Samia Suluhu Hassan, sambamba na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi, katika viwanja vya Tanganyika Packers, jijini Dar es Salaam jana Agosti 28, 2025.
Wakati CCM ikiendelea na kampeni mikoani, Chama cha NRA inatarajiwa kuwa mkoani Kigoma kuomba kura kwa ajili ya mgombea wake wa urais, Hassan Almas na mgombea mwenza wake, Hamis Majukumu.
Chama cha ADC nacho kimepangwa kuelekeza kampeni zake jijini Mwanza, kikimnadi mgombea wake wa urais, Wilson Mulumbe na mgombea mwenza wake, Shoka Juma.
Leo, Agosti 29, 2025, CCM imehamia Morogoro ambako yupo mgombea urais, huku mgombea mwenza, Dk Nchimbi, akiendelea na kampeni jijini Mwanza.
Wakati huohuo, mgombea urais wa NRA, Hassan Almas, anatarajiwa kuendelea na kampeni zake mkoani Mtwara, huku mgombea mwenza wake, Hamis Majukumu, akiwafuata wananchi wa Mkoa wa Tanga.
Agosti 30 mgombea huyo wa urais wa NRA atahamia mkoani Ruvuma huku mgombea mwenza wake, akihamia Dar es Salaam.
Pia siku hiyo, mgombea urais wa ADC na mgombea mwenza, wanapaswa kuzisaka kura mkoani Tanga, huku Chama cha CCK kikitarajiwa kufungua pazia la kampeni mkoani Dar es Salaam.
Siku inayofuata, Agosti 31 mgombea urais wa CCM, Samia ataenda kunadi sera kwa wananchi mkoani Dodoma, huku mgombea mwenza akiendelea na kujinadi Kanda ya Ziwa, katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wa NRA, safari inatarajiwa kuhamia Mbeya kwa mgombea urais, huku mgombea mwenza akivuka maji hadi Kaskazini Pemba, Zanzibar.
Agosti 31, 2025 Chama cha AAFP kinatarajiwa kuzindua kampeni zake mkoani Morogoro kikiwakutanisha mgombea urais, Kunje Ngombare-Mwiru na mgombea mwenza, Chumu Juma.
Chama cha Wananchi (CUF), kwa mujibu wa ratiba hiyo kinapaswa siku hiyo kuzindua kampeni zake jijini Mwanza, kikiwahusisha mgombea urais Samandito Gombo na mgombea mwenza ni Husna Abdulla.
Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), siku hiyohiyo pia kitazindua kampeni zake kuwanadi Salum Mwalimu, mgombea urais na mgombea mwenza, Devotha Minja, jijini Dar es Salaam.
Mgombea urais na mgombea mwenza wa ADC, kwa siku hiyo wataweka kambi Jiji la Tanga kuzisaka kura za urais.
Septemba mosi, 2025 itakuwa mapumziko kwa mgombea urais wa CCM, wakati mgombea mwenza akiendelea kuchanja mbuga Mkoa wa Simiyu.
Siku hiyohiyo, itaakuwa fursa kwa mgombea urais wa Chaumma kujinadi mkoani Tanga, wakati mhombea mwenza, Devotha akiendelea na kazi hiyo mkoani Morogoro eneo ambalo watakuwepo pia wagombea wa AAFP.
Wagombea wa CUF, watakuwa mkoani Mara, siku ambayo mgombea urais wa UDP, Saum Rashid na mgombea mwenza, Juma Faki wakiwa mkoani Mwanza.
Kwa upande wa wagombea wa ADC, siku hiyo ya Septemba mosi watakuwapo Mkoa wa Tanga, huku NLD ikitarajiwa kuzindua kampeni zake mkoani Dar es Salaam, kumnadi mgombea urais, Hassan Doyo na mgombea mwenza, Chausiku Mohammed.
Mgombea urais wa NRA siku hiyo atakuwa mkoani Iringa, huku mgombea mwenza wake akiwa Mtwara.
Septemba 2, 2025 mgombea mwenza wa CCM ataendelea kuomba kura mkoani Simiyu na AAFP ikiwa Morogoro. Mgombea urais wa Chaumma anakuwa Tanga huku mgombea mwenza wake akisalia nyumbani mkoani Morogoro.
Wagombea wa CUF watakuwa Mara, huku mgombea urais wa Demokrasia Makini, Coaster Kibonde na mgombea mwenza, Azza Suleiman wakitarajiwa kuzindua kampeni jijini Dar es Salaam.
Siku hiyohiyo, UDP itakuwa mkoani Simiyu, ADC mkoani Tanga na Kilimanjaro, NLD Dar es Salaam, huku mgombea urais wa NRA akiwa Morogoro na mgombea mwenza Mkoa wa Ruvuma.
Septemba 3, 2025 mgombea urais wa CCM atahamia Songwe, wakati mgombea mwenza akiendelea kuomba kura Simiyu na kisha Shinyanga.
Siku hiyo inatarajiwa kuwa mwanzo wa kampeni za urais za Chama cha CCK kwa mgombea wake, David Mwaijolele na mgombea mwenza, Masoud Ally.
Mgombea urais wa Chaumma atakuwa Tanga na Kilimanjaro, huku mgombea mwenza akiwa Morogoro.
Wagombea wa CUF watakuwa Simiyu, huku wale wa UDP wakiwa Mara, Demokrasia Makini Pwani, ADC Kilimanjaro na NLD jijini Dar es Salaam.
Mgombea urais wa NRA ataihitimisha wiki ya kwanza ya kampeni kwa kuomba kura mkoani Kagera, huku mgombea mwenza akitarajiwa kuwa Ruvuma.