Hekima ya Sunna ya Aqiqa katika Uislam

Dar es Salaam. Aqiqa” ni mnyama anayechinjwa kwa ajili ya mtoto wa kiume au wa kike siku ya saba baada ya kuzaliwa, kwa ajili ya kumshukuru Allah Mtukufu.

Ibada hii ni Sunna muhimu katika Uislamu ambapo familia inafurahi kwa kupata mtoto mpya.

Ushahidi wa Sunna hii ni kauli ya Mtume wa Allah (Rehema na amani ziwe juu yake):

“Kila mtoto amefungika na ibada ya Aqiqa, huchinjiwa mnyama siku ya saba (toka azaliwe), hunyolewa na kupewa jina siku hiyo” (At-Tirmidhi).

Kwa mujibu wa madhehebu yetu ya Shafii ibada hii ni Sunna iliyosisitizwa na kutiliwa mkazo. Lakini hakuna dhambi kwa anayeiacha. Ushahidi wa Sunna hii ni kauli ya Mtume wa Allah:

“Atakayezaliwa mtoto wake na akapenda kumfanyia ibada ya kuchinja (Aqiqa), basi na achinje; kwa mtoto wa kiume kondoo (au mbuzi) wawili waliojitosheleza, na kwa mtoto wa kike kondoo (au mbuzi) mmoja.”

Hii inaonyesha kuwa ibada ya Aqiqa ni jambo la sunna iliyosisitizwa na wala si jambo la wajibu na lazima. Ni bora kuchinjwa siku ya saba, na ikiwa imechelewa, inafaa kufanyiwa mtoto wakati wowote, na hakuna dhambi kwa kuchelewesha.”

Hikma ya ibada ya Aqiqa imeelezwa katika kauli ya Mtume wa Allah: “Kila mtoto amefungika na ‘Aqiqa yake.”Wanazuoni wameeleza ikiwa hakufanyiwa na akafariki akiwa mtoto, basi atazuiliwa kuwapa wazazi wake uombezi (shafaa).

Ibada ya Aqiqa ni kinga dhidi ya shetani na njia ya kumlinda mtoto, na huenda mtoto akakosa kheri kutokana na uzembe wa wazazi wake. Ibn al-Qayyim (Allah amrehemu) ameeleza baadhi ya faida za ibada ya Aqiqa, ni sadaka inayotolewa kwa ajili ya mtoto katika siku za mwanzo za kuzaliwa kwake. Aqiqa ni njia ya kuwaleta pamoja jamaa na marafiki katika karamu. .

Ni Sunna ibada ya Aqiqa kuchinjwa kwa ajili ya mtoto siku ya saba baada ya kuzaliwa kwake. Wanazuoni wametofautiana mitazamo yao kuhusu siku ya kuzaliwa, je inahesabiwa katika siku saba au la?

Jopo la wanazuoni wa Sharia ya Kiislamu (Al-Jumhur) wamesema siku ya kuzaliwa inahesabiwa ikiwa mtoto amezaliwa mchana, basi siku hiyo huhesabiwa. Ikiwa amezaliwa usiku, basi huanza kuhesabiwa siku inayofuata. An-Nawawi amesema: “Kama atachinjwa baada ya siku ya saba au kabla yake baada ya kuzaliwa, inakubalika. Lakini ikichinjwa kabla ya kuzaliwa haitakubalika, bali itakuwa ni nyama ya kawaida tu.”

Bora zaidi ni kumchinja katika mji wa mtoto, hata kama baba yupo mbali, basi atume gharama na amuagize mtu achinje, ili watu wamuombee dua mtoto na kumpongeza.” Inafaa pia kuchinja mbuzi mmoja hapa na mwingine kwingineko, ili kuleta furaha kwa pande zote za jamaa.

Kiasili,Aqiqa ni jukumu la baba wa mtoto, na si katika mali ya mama, wala ya mtoto mwenyewe. Lakini wanazuoni wameruhusu watu wengine kumfanyia mtoto Aqiqa kwa masharti, ikiwa baba amekataa au amepuuzia. Au mtu ameomba ruhusa ya baba, naye akakubali.

Sunna imehimizia Aqiqa kwa kila mtoto bila kubagua hata wa zinaa. Hivyo, hata mtoto wa zinaa hujumuishwa. Kwa kuwa mtoto huyu anahusishwa na mama yake, basi mama ndiye atakayefanya Aqiqa akiwa ana uwezo, na kutubu kwa Allah kutokana na dhambi aliyoifanya ya zinaa.

Wanazuoni wengi wameruhusu ngamia na ng’ombe, kwa kuwa wanahesabiwa kama wanyama wanaokubalika katika udh,hiya. Lakini bora zaidi ni kondoo au mbuzi kwa kuwa ndio waliothibitishwa kimaalum katika Sunna hii.

Sharti za mnyama wa Aqiqa ndio zile zile za mnyama wa Udh.hiya (anayechinjwa katika siku ya sikukuu ya Mfungotatu). Asiwe na dosari, awe amefikia umri unaokubalika (miaka 5 kwa ngamia, miaka 2 kwa ng’ombe, mwaka 1 kwa mbuzi, miezi 6 kwa kondoo). Haikubaliki mnyama mwenye upofu wa wazi, ulemavu mkubwa, ugonjwa wa dhahiri, au udhaifu uliopitiliza. Na wala hailazimiki kutajwa jina la mtoto wakati wa kuchinja, bali inatosha nia ya mzazi kuwa hii ni ibada ya Aqiqa. Na wala hakuna mgawanyo maalumu katika Sunna hii. Kile kilichowekwa kipaumbele ni kuchinja.

Ibn Qudama na wanazuoni wengine walieleza kuwa muhusika ana uhuru wa kula, kugawa au kutokula. Sheikh al-Albani amesema: anaweza kula yote, kutoa yote kwa maskini, au kula na kugawa sehemu.

Masuala yanayohusiana na Aqiqa

Kama mimba imeharibika kabla ya kufikia miezi minne (4), hakuna aqiqa, kwa kuwa bado roho haijapuliziwa kwa mtoto. Ikiwa mimba imeharibika baada ya miezi minne (4): Wanazuoni wamekhitalifiana, lakini kauli iliyo sahihi ni kwamba inapendekezwa kufanyiwa aqiqa.

Pia mtoto huyo huoshwa, hufunikwa sanda, huswaliwa na kuzikwa pamoja na Waislamu. Madhehebu ya Hanbali walikataza kuchanganya aqiqa kwa watoto wengi kwa mnyama mmoja (mfano: ng’ombe mmoja kugawanywa kwa watoto saba). Walisema Aqiqa ni fidia ya nafsi ya mtoto mmoja, hivyo kila mtoto anahitaji mnyama wake kamili (mbuzi mmoja au wawili).