Kesi ya mtoto wa Askofu Sepeku dhidi ya Kanisa la Anglikana kuunguruma tena leo

Dar es Salaam. Kesi ya Bernardo Sepeku ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku aliyekuwa Askofu  wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, inaendelea leo Ijumaa, Agosti 29, 2025 Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi.

Bernardo amefungua kesi mahakamani hapo, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Amefungua kesi hiyo ardhi namba 378/2023, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Angilana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Hivyo katika madai yake, pamoja na mambo mengine anaomba alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa ardhi katika kiwanja hicho.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa leo Ijumaa Agosti 29, 2025 mbele ye Jaji Arafa Msafiri anayesiliza shauri hilo, ambapo Askofu Johnson Chinyong’ole (63) wa Dayosisi ya Shinyanga, atahojiwa maswali ya kusawazisha na wakili wake baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake dhidi ya Sepeku.

Sepeku anatetewa na mawakili wawili ambao ni Deogratias Butawantemi  na Gwamaka Sekela huku wajibu maombi wao wanatetewa na wakili Dennis Malamba.

Tayari mashahidi watatu wa wajibu maombi wameshajitetea mahakamani hapo.

Miongoni mwao ni Katibu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mchungaji George Lawi ambaye alitoa ushahidi wake dhidi ya mleta madai (Sepeku).

Katika utetezi wake aliyoutoa Julai 18, 2025, Lawi aliikana Katiba ya kanisa hilo ambayo ni kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo ya mgogoro wa zawadi ya shamba na nyumba alizopewa  Askofu Mkuu wa kwanza wa kanisa hilo nchini, John Sepeku.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa madai uliotolewa na mashahidi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na maaskofu wengine wa kanisa hilo, Askofu Sepeku alipewa zaidi hiyo na Dayosisi ya Dar es Salaam mwaka 1980.

Pendekezo la kumzawadia Askofu Sepeku shamba na nyumba lilitolewa awali na Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao chake cha Desemba 8, 1978.

‎‎Sinodi ya Dayosisi hiyo katika kikao chake cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia na kuazimia kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi, shamba la eka 20 lililoko Buza wilayani Temeke, Dar es Salaam, na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mchungaji Lawi ambaye aliieleza Mahakama hiyo, kuwa pia ni Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo Nchini (mdaiwa wa kwanza) katika ushahidi wake, alikana kutambua shamba na nyumba hiyo kutolewa kwa Askofu Sepeku kama zawadi.

Vilevile, katika utetezi wake, Askofu Chinyong’ole alidai kikao cha Sinodi sio chombo cha kutoa zawadi kwa sababu hakina mamlaka na hata zawadi ya kiwanja aliyopewa marehemu Sepeku, haikufuata taratibu licha ya kukiri kuwa kikao hicho ndicho chombo cha mwisho cha kutoa maamuzi ambayo hayawezi kupingwa na vikao vingine vya kanisa.

Hata hivyo, alipohojiwa na wakili Gwamaka Sekela na Deogratias Butawantemi wa mleta maombi katika shauri hilo kuhusu utaratibu uliotakiwa kufuatwa ili Sepeku apewe zawadi hiyo, shahidi huyo alishindwa kufafanua utaratibu huo.

Endelea kufuatilia Mwananchi