KIPA tegemeo wa timu ya JKU, Ahmed Issa amezimwaga timu tatu kisiwani hapa ambazo zilikuwa zinahitaji huduma yake huku akisema sababu ya kufanya hivyo anasubiri usajili wa dirisha dogo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofunguliwa Desemba mwaka huu ili avuke maji kusaka malisho mapya.
Amesema, anafanya hivyo kwa sababu malengo yake ni kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara ndio maana amekataa ofa ya timu hizo na kubaki JKU akitambua kuwa hapo ndio sehemu sahihi kwake kwa sasa.
Timu ambazo zilikuwa zinamuhitaji kipa huyo na kuamua kukataa ofa zao ni KVZ, Mwembe Makumbi na Mafunzo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ahmed amesema bado ana matumaini ya kuwa ana uwezo wa kucheza Ligi Kuu Bara ndio maana anaendelea kusubiri hadi utakapofika usajili wa dirisha dogo msimu wa 2025-2026.
“Nimefanya uamuzi wa kubaki JKU lengo langu ni kucheza nje ya Zanzibar hivyo kwa sasa sihitaji kuingia mikataba na timu nyingine kisiwani hapa ingawa ofa zao zilikuwa nzuri kwangu lakini sipo tayari,” amesema Ahmed.
Hata hivyo, licha ya timu za Tanzania Bara kutojitokeza kutaka huduma ya kipa huyo katika usajili wa dirisha kubwa uliofunguliwa Julai 1, 2025 na kutarajiwa kufungwa Septemba 7, 2025, anasema bado atasubiri usajili wa dirisha dogo.