Kipa wa Simba kutua Tabora United

MABOSI wa Simba leo Ijumaa walitarajia kufanya kikao cha kumalizana na mmoja wa makipa waliokuwa wakiitumikia timu hiyo, ikidaiwa mipango ya kumtoa kwa mkopo imekuwa ngumu baada ya kipa huyo kugoma na kutaka alipwe chake asepe mazima Msimbazi.

Hatua hiyo, imewafanya mabosi wa Simba kuitisha kikosi hicho cha jana kwa lengo la kumalizana na kipa huyo ili mambo mengine yaendelee, huku timu hiyo ikiwa imejihakikisha kumbeba Yakoub Suleiman aliyekuwa JKT Tanzania.

Salim bado ana mkataba wa miaka mitatu na Simba baada ya awali kusainishwa miaka mitano na kuitumikiwa miwili tu hadi mssimu uliopita na kipa huyo aliyezaliwa Aprili 19, 2000 Pemba visiwani Zanzibar hakuwa katika mpango wa sehemu wa kikosi hicho kwa msimu mpya wa 2025-2026.

Chanzo cha ndani kilisema Simba ilitaka kumtoa kwa mkopo Salim kwenda Namungo, lakini kipa huyo hakuwa tayari kwenda huko na badala yake anataka uvunjwe mkataba na alipwe chake.

“Mchezaji anaonekana hataki atolewe kwa mkopo maana mbali na Simba kutaka kumpeleka Namungo, kulikuwepo na mpango wa kumpeleka JKT Tanzania, baada ya kuona imeshindikana JKT ikamsajili Ramadhan Chalamanda kutoka Kagera Sugar,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Simba inaangalia namna nzuri ya kumalizana kwa amani na kipa huyo iliyokaa naye kwa muda mrefu, tangu akiwa kikosi B, ili kumpa nafasi ya kwenda kupata changamoto mpya ya kazi yake.”

Mwanaspoti limepata taarifa za ndani za Salim huenda akatua Tabora United kulikuwepo na mazungumzo baina yao yalikuwa yanaendelea, lakini yalishindwa kufikia mwafaka kutokana na mkataba alionao Simba.

“Kama mambo yake yakienda sawa, huenda akajiunga na Tabora ndiyo iliyokuwa inafanya naye mazungumzo na yalifikia pazuri ila ilisita bado mchezaji huyo ana mkataba na Simba,” kilisema chanzo hicho.