Kipimo cha usajili kipo robo fainali

WAKATI timu zikipambana kutafuta nafasi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), hali inaonyesha timu itakayotoboa ni ile iliyofanya usajili wa wachezaji wenye viwango vikubwa.

Hiyo imetokana na ushindani mkubwa uliokuwepo kwa timu tano, zinazo tafuta nafasi za kucheza robo fainali ambapo Dar City, Jeshi Stars na JKT Stars ndizo zilizotangulia kushinda na kwenda nusu fainali.

Timu nyingine za JKT, Savio, UDSM Outsiders, Stein Warriors, Pazi na ABC pia zinapambana kutafuta nafasi hiyo.

Kwa upande wanawake timu zinazotafuta nafasi hiyo ni; Tausi Royals, DB Lioness, DB Troncatti na Polisi Stars. 

Kwa upande wa Dar City, iliyosheheni wachezaji wenye viwango vya juu, imekuwa ikizipa wakati mgumu timu pinzani kushinda.

Wachezaji waliowezesha timu hiyo kuingia nusu fainali ni, Sharom Ikedigwe, Clinton Best (Nigeria), Jamel Marbuary (Marekani) na Victor Mwoka (Kenya).

Nyota hao walishirikiana vizuri na wachezaji wazawa ambao ni Amin Mkosa, Ally Abdallah, Fotius Ngaiza na Ally Faraji.

Kwa upande wa Jeshi Stars, imeonyesha imejipanga vizuri ni baada ya kusajili wachezaji wenye uwezo wa juu ambao ni Anamary Cyprian, Monalisa Kaijage Witness Mapunda, Noela Uwendameno na Bhoke Juma wakishirikiana na mkongwe Faraja Malaki. 

Upande wa JKT Stars inajivunia wachezaji wake hususani waliokaa pamoja kwa muda mrefu, akiwamo Jesca Ngisaise, Wade Jaha, Doritha Mbunda na Sara Budodi.

RB 01

Mchezo kati ya Dar City na Srelio ulikuwa ni wenye ushindani mkubwa na ubora wa timu ya Dar City uliifanya iibuke na ushindi.

Srelio iliyokuwa na wachezaji nyota kutoka Gabon, Junior Louissi na Lerry Mve ilishindwa kukabiliana na wachezaji wa Dar City, ambayo imetinga nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa michezo 2-0.

Katika mchezo wa kwanza Dar City ilishinda kwa pointi 90-53 na ule wa pili ikashinda kwa pointi 93-72.

Timu ya Jeshi Stars iliingia nusu fainali baada ya kuifunga Pazi Queens kwa ushindi wa jumla wa 2-0, kwani mchezo wa kwanza ilishinda kwa pointi 79-52 na mchezo wa pili ikashinda kwa pointi 63-53.

Katika mchezo huo wa pili Jeshi Stars iliongoza katika robo zote nne kwa pointi 15-11, 13-11, 18-16 na 17-15.

Katika mchezo huo, Anamary Cyprian alifunga pointi 16, akifuatiwa na Noela Uwendameno aliyefunga pointi 13.

Kwa upande wa Pazi Queens alikuwa Maria Mbena aliyefunga pointi 20, akifuatiwa na Maria Bonventura aliyefunga pointi 13.

RB 02

ABC YAWAFANYIZIA WAKONGWE PAZI

Ubora wa Ligi ya BDL ulidhihirika baada ya timu ya ABC kuifunga Pazi  kwa pointi 63-55,  katika robo fainali ya pili iliyofanyika kwenye Uwanja wa Donbosco, Upanga.

Katika mchezo wa kwanza wa robo fainali hiyo,  Pazi ilishinda kwa pointi 63-50, iliyofanya timu hizo zifungane mchezo mmoja mmoja.

Robo fainali hiyo inachezwa kwa  timu kucheza michezo mitatu (best of three playoffs), mchezo wa tatu utakaochezwa keshokutwa (Jumapili) ndiyo utakaoamua timu itakayoingia nusu fainali.

Katika robo fainali ya pili, timu ya Pazi iliingia uwanjani huku ikijiamini kutokana na kumbukumbu ya ushindi ilioupata katika robo fainali ya kwanza, huku timu ya ABC ikicheza kwa lengo la  kutaka kurudisha kisasi cha kufungwa na Pazi katika mchezo wa kwanza.

Katika mchezo huo, Alinani Msongole alikuwa mwiba kwa timu ya Pazi, kutokana asisti zake alizokuwa anatoa kwa mfungaji.

Elias Nshishi akiongoza kwa kudaka mipira yote (rebounds) katika eneo lake,  huku upande wa timu ya Pazi walioonyesha kiwango kizuri walikuwa ni Soro Geoffrey, Victor Michael na Josephat Peter.

RB 03

JKT STARS v VIJANA QUEENS

Timu ya JKT Stars ilitinga nusu fainali baada ya kuifunga timu ngumu ya Vijana Queens katika michezo 2-0.

JKT iliyowakilishwa na nyota wake wote, katika mchezo wa kwanza ilishinda kwa pointi 52-36, na mchezo wa pili ikashinda kwa pointi 70-61.