Lishe inavyoathiri hisia, afya ya akili

Watu wengi wanapozungumzia lishe, mawazo huenda moja kwa moja kwenye uzito wa mwili, nguvu za mwili au maumbile ya nje kama vile ngozi, nywele na misuli. 

Hata hivyo, kuna upande mwingine muhimu wa lishe ambao haupewi uzito wa kutosha, nao ni ule wa athari zake kwenye hisia na afya ya akili.

 Lishe unayokula kila siku huchangia kwa kiasi kikubwa jinsi unavyojihisi: kama una furaha au huzuni, kama una msongo au utulivu, na hata kama una nguvu za kiakili au uko legelege.

Mwili na akili ni kitu kimoja, na kile unachoweka tumboni kina uwezo wa kuamuru kinachotokea kichwani.

Hisia ni matokeo ya mchanganyiko wa vichocheo vya mwili, mazingira, na hali ya akili.

Ofisa lishe wa Mkoa wa Mwanza, Sophia Lugome, anasema lishe bora ni muhimu si tu kwa afya ya mwili, bali pia kwa afya ya akili na hisia.

Anaeleza kuwa virutubisho vinavyopatikana katika mlo bora husaidia katika ukuaji wa afya ya akili, ubongo na hisia.

 “Ulaji wa vyakula vyenye virutubisho muhimu husaidia kuboresha utendaji wa ubongo na kupunguza hatari ya matatizo ya akili,”anasema.

Sophia anaeleza virutubisho kama vitamini B, na madini ya chuma ni muhimu kwa afya ya ubongo, huku akiongeza  kuwavyakula vyenye wanga tata, protini za kutosha, na mafuta yenye afya husaidia katika utendaji wa akili na hisia.

“Lishe bora ni msingi wa afya ya akili na ubongo, na inachangia katika kupunguza viashiria vya msongo na unyogovu,”anaeleza.

Aidha, anasema kuwa ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta yaliyojaa,  unaweza kuathiri afya ya akili na hisia kwa kuwa vyakula hivyo vinaweza kuongeza hatari ya kupata matatizo ya akili kama vile wasiwasi.

“Lishe bora ni silaha muhimu katika kujikinga na matatizo ya akili na hisia. Kila mmoja anapaswa kuchukua hatua za kuboresha mlo wake ili kufikia afya bora ya akili na mwili,”anasema na kuongeza:

“Makundi ya vyakula ni muhimu kwa sababu hutoa virutubisho vinavyohitajika kwa ajili ya ukuaji, kinga ya mwili, na utendaji mzuri wa mwili na akili. Kwa mfano, mbogamboga na matunda hutoa vitamini na madini muhimu, nafaka zisizokobolewa hutoa nyuzinyuzi na nishati, na protini husaidia katika ujenzi wa tishu za mwili.’’

Anasema lishe bora  inaboresha afya ya akili kwa kusaidia kazi ya ubongo na kupunguza hatari ya magonjwa ya akili kama vile unyogovu na Alzheimer (ugonjwa wa ubongo unaoathiri kumbukumbu, uamuzi, na uwezo wa kufikiri).

Katika utafiti wa kisasa wa sayansi ya lishe na afya ya akili, wanasayansi wamegundua kuwa chakula kina uhusiano wa moja kwa moja na kemikali za ubongo kama vile serotonin, dopamine na cortisol, ambazo zote zinaathiri hali ya mtu kihisia.

Serotonin ni kemikali maarufu inayohusiana na furaha, usingizi mzuri, na utulivu wa kihisia. Inashangaza kwamba asilimia kubwa ya serotonin (takriban asilimia 90) huzalishwa tumboni siyo kwenye ubongo kama wengi wanavyodhani.

Hii ina maana kuwa afya ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula ina nafasi ya moja kwa moja kwenye utengenezaji wa kemikali hii ya furaha.

Vyakula vyenye virutubisho kama vile tryptophan (ambavyo hupatikana kwenye mayai, maharagwe, karanga na mbegu), pamoja na vyakula vyenye bakteria hai  kama mtindi  husaidia kuongeza uzalishaji wa serotonin.

Wakati huo huo, ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi na wanga rahisi  kama soda, keki, mikate meupe na biskuti, una uwezo wa kuleta hisia za furaha ya muda mfupi kisha kuanguka kwa ghafla kwa hisia hizo. Sukari husababisha mlipuko wa ghafla wa insulin, ambao huweza kuongeza dopamine (kemikali ya “motisha”) kwa haraka, lakini athari yake huwa ya muda mfupi.

Baada ya hapo, mwili huingia katika hali ya kuchoka, huzuni, na hata wasiwasi. Hili linaweza kueleza kwa nini watu wengine hujikuta wanakula zaidi wanapokuwa na huzuni, kwani wanatafuta faraja ya haraka bila kujua kuwa wanazidisha hali hiyo hiyo wanayoikimbia.

Mifano ya kila siku inaweza kusaidia kuelewa dhana hii zaidi. Fikiria kijana ambaye kila asubuhi anakunywa soda na kula maandazi.

Kisha mchana anakula chipsi na kuku wa kukaanga, na usiku anakula chakula kizito kilichopikwa kwa mafuta mengi na sukari nyingi.

Kijana huyu anaweza kushangaa kwa nini kila siku anajihisi mvivu, hana hamasa, au ana mawazo mengi yasiyoisha.

Ukweli ni kwamba mfumo wake wa chakula hautoi msaada wa kutosha kwa ubongo wake kufanya kazi kwa utulivu.

Bila madini na virutubisho muhimu kama omega-3, magnesiamu, vitamini B na antioxidants, ubongo unakuwa katika hali ya uhitaji wa kudumu, hali inayoweza kujitokeza kwa njia ya hasira, kukata tamaa, au kutoweza kuzingatia.

Vyakula vyenye omega-3, kama samaki wa maji baridi (hasa salmon), mbegu za chia na karanga, vina uwezo wa kupunguza msongo wa mawazo  na hata dalili za unyogovu.

Magnesiamu inayopatikana kwenye mboga za majani mabichi, maharagwe na parachichi husaidia mfumo wa neva kupumzika na kubeba ujumbe kutoka sehemu moja ya mwili kwenda nyingine. Hii husaidia kupunguza hali za wasiwasi na kuwafanya watu wajihisi salama zaidi kiakili.

Siyo tu kwamba lishe duni inaweza kusababisha mabadiliko ya hisia, bali pia inaweza kuchochea magonjwa ya akili kwa watu walio hatarini.

Kazi kadhaa za kitafiti  zimeonyesha kuwa watu wanaotumia vyakula vya haraka kwa kiwango kikubwa wana uwezekano mkubwa wa kupata unyogovu, hasa vijana.

Ingawa lishe si chanzo pekee cha magonjwa ya akili, ni kipengele muhimu kinachoweza kuchochea au kupunguza hatari.

Jambo lingine la kuzingatia ni jinsi ulaji usio na ratiba unavyoathiri hisia. Vijana wengi wa mijini hawana muda wa kula milo kamili; wanakula kwa haraka, ama wakiwa njiani au wakati wa kutumia simu.

Matokeo yake ni kukosa virutubisho muhimu na kuvuruga mfumo wa mwili wa njaa na kushiba. Wakati mwingine mtu anaweza kuwa na hasira au huzuni lakini chanzo ni njaa tu au kiwango kidogo cha sukari kwenye damu.

Pia, kunywa maji ya kutosha ni jambo linalopuuzwa lakini lina athari kubwa. Upungufu wa maji mwilini unaweza kusababisha uchovu wa akili, hasira zisizo na msingi na kupungua kwa uwezo wa kufikiri vizuri.

Ikumbukwe lishe si tu suala la kupata umbo zuri au kukwepa magonjwa ya mwili. Ni silaha ya nguvu ya kuimarisha afya ya akili na kudhibiti hisia.

Jinsi unavyokula leo inaamua jinsi utakavyojihisi kesho. Ikiwa unataka kuwa na akili tulivu, yenye nguvu, na furaha ya kweli, anza kwa kuangalia sahani yako. Kwa sababu mwishowe, unachokula kinaamua si tu umbo lako  bali pia hisia zako.