Madagascar, Sudan mmetupa somo CHAN

KIJIWE kilipoa sana baada ya Taifa Stars kutolewa na Morocco katika robo fainali ya mashindano ya CHAN 2024 ambayo kesho Jumamosi yatafikia tamati.

Hatuwezi kuchangamka na huku timu ambayo inasimama kama alama ya kutuunganisha Watanzania na mwenyeji, kuaga katika ardhi ya nyumbani.

CHAN imetufunza mengi na miongoni mwa masomo tumeyapata kwa timu mbili za Madagascar ambayo imeingia hatua ya fainali na timu ya Sudan ambayo yenyewe ilikwama katika nusu fainali.

Bahati nzuri timu hizo mbili zilikutana katika hatua ya nusu fainali na Madagascar ikapata ushindi wa bao 1-0 huku ikiwa na idadi pungufu ya wachezaji uwanjani kwa vile mchezaji wao mmoja alionyeshwa kadi nyekundu.

Masomo mawili ambayo tunayapata kutoka kwa timu hizo mbili ni uhitaji wa wachezaji walio bora kimbinu na makini na kucheza kwa kujitolea yanaweza kuwa silaha ya mafanikio katika soka.

Sudan wana muda mrefu bila ligi yao kuchezwa huku Madagascar ikiwa haina ligi yenye umaarufu au ukubwa kulinganisha na nchi nyingi ambazo zimeshiriki CHAN mwaka huu lakini zote zimefanikiwa.

Kwanza zina wachezaji ambao wanaweza kufanyia vyema mipango ya kimbinu ya makocha wao na kwa umakini mkubwa katika dakika zote za mchezo huku muda wote wakijituma kuhakikisha timu zao zinafanya vyema.

Kumbe inawezekana usiwe na ligi maarufu au iliyo juu katika chati ya ubora lakini ukaweza kutengeneza timu imara ya taifa ya wachezaji wa ndani ambayo itakubeba kama ambavyo Madagascar na Sudan zimefanya kwenye CHAN.

Zinatufundisha pia ubora wa Ligi kwenye chati za CAF kuna wakati haumaanishi kuwa timu ya taifa ya nchi husika ndio itakuwa nzuri kwa vile inawezekana hadhi hiyo ya ligi ikabebwa na wachezaji wa kigeni.