Madhara ya kubana haja ndogo muda mrefu

Dar es Salaam. Je, una tabia ya kubana mkojo kwa muda mrefu yani kuanzia saa tatu na kuendelea? Unajua ni kwa namna gani tabia hiyo ni hatarishi kwa afya yako na mfumo wa utoaji takamwili kwa ujumla?

Baadhi ya watu hubana mkojo kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali,  ikiwemo kutokuwa katika mazingira rafiki ya kupata huduma hiyo.

Wengine hufanya hivyo kwa mapenzi yao binafsi kutokana na kutojua athari zake. Hata hivyo wataalamu mbalimbali wa afya wameonya juu ya tabia hiyo,  wakisema inaweza kusababisha madhara kiafya, ikiwemo kujirudia mara kwa mara kwa changamoto ya maambukizi ya njia ya mkojo (U.T.I).

Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya Healthline mtu anatakiwa kutoa haja ndogo kila baada ya saa tatu hadi nne.

Akizungumza na Mwananchi,  Daktari wa binadamu, Shitta Samweli anasema tabia ya kubana mkojo hasa inapofanywa mara kwa mara,  inaweza kusababisha U.T.I kujirudia mara kwa mara,  kwa sababu kadri unavyobana mkojo ndivyo bakteria wasiofaa wanavyozidi kuzaliana na kusababisha kuwa wengi na kuleta athari katika mfumo wa mkojo.

Anasema wanawake wapo katika hatari zaidi ya kupata changamoto hiyo kuliko wanaume kutokana na muundo wa mfumo wao wa mkojo.

“Kadri unavyobana mkojo kwa muda mrefu ndivyo unavyowapa bakteria muda na mazingira ya kuzaliana kwa wingi ndani ya kibofu,  hivyo kusababisha changamoto ya maambukizi katika njia ya mkojo (U.T.I) na hili hujitokeza zaidi kwa wanawake, ”anasema.

Dk Shitta anasema tabia hiyo inaweza kumweka mtu katika hatari ya kupata matatizo ya figo ikiwemo kupata mawe katika figo.

“Mkojo ni uchafu ambao unatakiwa utoke,  kuendelea kuuhifadhi kwenye kibofu kwa mda mrefu ni  kumweka mtu katika hatari ya kupata maradhi ya figo, ”anasema.

Pia anasema tabia hiyo inaweza kuathiri kibofu na kusababisha misuli yake kulegea na hata kuharibu mfumo wa utendaji kazi kati ya ubongo na kibofu.

“Kutokana na kuharibika kwa mfumo wa mawasiliano kati ya ubongo na kibofu kuharibika huweza kusabisha mtu kushindwa kuzuia mkojo” anasema.

Kwa upande wake,  Dk Daudi Gambo anasema athari nyingine zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kupata majeraha katika kibofu kutokana na mkojo kuwa na asili ya asidi

Anaongeza kuwa athari hizo zinaweza zisionekane kwa haraka, kwani mara nyingi hujitokeza mtu anapokuwa mtu mzima.

Dk Gambo anashauri wenye tabia ya kubana mkojo muda mrefu kuacha mara moja kwani inaweza kuwaletea athari hasa wanapofika umri wa uzee.

Anasema ni muhimu kila mtu kama yupo katika mazingira rafiki kuhakikisha anatoa haja ndogo kila baada ya saa tatu.

Hata hivyo,  kwa mujibu wa tovuti ya Healthline humchukua takribani saa 1-2 kwa mtoto wa umri 0 hadi miezi 12 kibofu chake kujaa mkojo.

Mwenye umri wa mwaka mmoja hadi minne humchukua saa mbili hadi tatu kibofu kujaa.

Kuanzia umri wa miaka minne na kuendelea huchukua saa mbili hadi nne kibofu cha mkojo kujaa.

Mambo mengine aliyoshauri kuzingatiwa ili mfumo wa mkojo uwe na afya na kutenda kazi vizuri,  ni pamoja na unywaji wa maji ya kutosha, kuzingatia usafi wa mwili, nguo za ndani  na vyoo pamoja na lishe bora.

Anaongeza kuwa pale mtu anapojihisi dalili mbalimbali zinazoashiria changamoto katika mfumo wa mkojo ikiwemo kupata maumivu wakati wa kutoa haja ndogo, kutoa mkojo wenye rangi ya chai na harufu kali, homa, maumivu ya kiuno na nyinginezo,  ni vyema kuwahi hospitali kupatiwa matibabu na kujiepusha na unywaji wa dawa kiholela bila ya kufika hospitali.

“Kuna baadhi ya watu wanapohisi tu dalili zinazoashiria changamoto ya kiafya hukimbilia kunywa dawa bila ya kwenda hospitali kufanyiwa vipimo na kupata ushauri wa daktari. Hii  ni hatari kwani inaweza kukufanya kutopata tiba stahiki ambayo itasababisha ugonjwa huo kujirudia tena au kutengeneza usugu wa dawa, “anaeleza.