WAKATI Simba ikirejea nchini alfajiri ya leo ikitokea Misri, mastaa wa timu hiyo wameringia usajili wa kikosi hicho kwa msimu msimu mpya wakisisitiza wamepania kufanya mabadiliko.
Simba iliweka kambi jiji la Ismailia kabla ya kuhamia Cairo, Misri ikitumia siku 31 kujifua tayari kwa msimu wa 2025/26 ambao utaanza rasmi Septemba 16 kwa kupigwa mechi ya Ngao ya Jamii itakayowakutanisha Wekundu wa Msimbazi hao dhidi ya watetezi, Yanga.
Wakizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kuwasili nchini, mshambuliaji Steve Mukwala, aliyekuwa na timu hiyo tangu msimu uliopita, alisema kwa sasa kikosi hicho kipo tayari kwa kuitafuta mafanikio ya msimu ujao.
Mukwala raia wa Uganda, alisema usajili mpya uliofanywa na timu hiyo utabeba nguvu kubwa ya mageuzi kwa msimu ujao akiridhishwa na wale waliosajiliwa dirisha hili kubwa la usajili.
Mshambuliaji huyo aliyemaliza msimu uliopita na mabao 13 sawa na Jonathan Sowah aliyekuwa Singida Black Stars, Leonel Ateba aliyepo kwa sasa Iraq na Prince Dube wa Yanga, aliongeza kwa namna kikosi hicho kilivyofanyiwa usajili pamoja na mazoezi waliyoyapata hawana sababu ya kushindwa kukosa mafanikio kwa msimu ujao.
“Tumekuwa na maandalizi mazuri, kuanzia tulipotoka hapa hadi hivi sasa tunaporejea, kila kitu kimefanyika kwa umakini mkubwa, naweza kusema tumekuwa na maandalizi mazuri kwa msimu mpya,” alisema Mukwala na kuongeza;
“Usajili mpya umefanyika kwa kiwango kikubwa, kila mmoja hapa ana furaha na aina ya wachezaji ambao wameongezwa kwenye timu, sisi waliotukuta, tumewapokea vizuri ili tushirikiane kuipa mafanikio Simba.
“Hakuna presha lakini ninachoweza kusema ni timu imeimarika, kama nilivyosema wachezaji waliokuja ni wazuri kwahiyo ushindani wa nafasi ndio ambao utakwenda kuipa faida timu, tuliyonayo sasa sidhani kama tuna sababu ya kukosa mafanikio kwa msimu ujao, tupo tayari.”
Msimu uliopita, Mukwala alimaliza na mabao 13 sawa na aliyekuwa mshambuliaji mwenzake wa timu hiyo Leonel Ateba, huku kinara wa ufungaji katika timu hiyo na Ligi Kuu akiwa ni kiungo wa Wekundu hao Charles Jean Ahoua aliyemaliza na mabao 16.
Wakati Mukwala akiyasema hayo mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Jonathan Sowah aliongeza ana imani kubwa na kikosi cha wekundu hao kwa msimu ujao.
Sowah ambaye alisajiliwa na Simba dirisha hili akitokea Singida Black Stars, alisema tayari wameshaanza kuzoeana uwanjani baina yao wachezaji akisema vipaji ndani ya kikosi chao ni vya hali ya juu.
“Nina imani kubwa sana na timu yetu,wachezaji niliowakuta na sisi ambao tumeongezeka naweza kusema tutakuwa na timu bora, kuanzia nilipofika mpaka sasa tumerejea, tupo tayari kwa mwanzo mpya wa mashindano,” alisema Sowah raia wa Ghana.
Msimu uliopita Sowah alifunga mabao 13 akitumia mechi 14 za duru la pili alizoitumikia Singida Black Stars, akiweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi akitumia nusu msimu tu.