Mauaji Ukraine vifo vyafika 23, serikali yatangaza siku ya maombolezo

Kyiv. Mamlaka za kiusalama nchini Ukraine zimesema jumla ya watu 23 wamefariki dunia na 48 wamejeruhiwa kufuatia shambulio la Urusi lililofanywa katika mji wa Kyiv siku ya jana.

Ifahamike kuwa mapema asubuhi ya jana jeshi la Urusi lilifanya shambulio lililohusisha ndege zisizo na rubani 598 na makombora 31 ya aina tofauti na likilenga maeneo 33 katika Wilaya za jiji hilo.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa utawala wa jiji la Kyiv Tymur Tkachenko, imesema miongoni mwa waliofariki ni watoto wanne na kila kitu kimeharibiwa ndani jiji hilo ambalo linakabiliwa na mashambulizi makubwa ya serikali ya kigaidi ya Urusi.

“Ni unyama, unaogonga raia, wengi wako katika hali mbaya, na madaktari sasa wanapigania maisha yao,” amesema Tkachenko.

Ofisa huyo ameongeza kuwa, majengo 100 ya mji huo yameharibika kutokana na milipuko mikali makombora ya Urusi yaliolenga  maeneo 33 katika wilaya zote 10 za jiji hilo yakiwemo makao makuu ya umoja wa Ulaya.

Meya wa jiji hilo Vitali Klitschko amesema siku ya leo Ijumaa itakuwa ya maombolezo na bendera zitashushwa kwenye majengo yote ya umma.

Klitaschko pia alitangaza kupiga marufuku hafla zote za umma  zote  za umma kwenye ofisi hizo hadi pale itakapotolewa taarifa nyingine.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuweka shinikizo kubwa zaidi kwa Urusi, ikiwa ni pamoja na vikwazo vipya, vikali, ikiwemo kuwatenga washirika wa Moscow na China.

Amesema washirika hao ni sababu ya kukwama kwa juhudi za Rais  Trump ambaye amekuwa akimshawishi Putin kusitisha vita vyake dhidi ya Ukraine, ili kutoa nafasi ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya Moscow na Kyiv.

Zelenskyy pia  alituma rambirambi zake kwa wapendwa wa waathiriwa na kusema tukio hilo ni jibu la wazi kwa kila mtu ulimwenguni ambaye, kwa wiki na miezi, amekuwa akitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na diplomasia ya kweli.

Mbali na hayo Ukraine  pia imeripotiwa  kufanya mashambulizi nchini Urusi kama ilivyoelezwa na Wizara ya Ulinzi ya Urusi ambayo imedai kudungua ndege zisizo na rubani za Ukraine zilizolenga maeneo saba ya nchi hiyo kwa usiku mmoja.

Mashambulizi hayo ya Ukraine yamesababisha zaidi ya watu 80  kuhama katika eneo hili  kutokana na uchafu unaoanguka kutoka kwenye ndege zisizo na rubani kaskazini mwa mkoa wa Rostov pamoja na uharibifu wa vinu viwili vya mafuta vya Urusi na kiwanda cha kusafisha mafuta cha Afipsky katika eneo la Krasnodar.

Elidaima Mangela (UDOM) kwa msaada wa Mashirika ya habari