Mstaafu anapotamani kurudisha kadi yake ya ustaafu!

Pamoja na miaka 66 aliyo nayo, mstaafu wetu anamiliki anachoita kitambulisho kimoja tu kinachomtambulisha kuwa yeye ni mstaafu wa shirika lililokuwa kubwa enzi zake la ‘nanihii’, alichopata siku alipostaafu kwa hiari yake miaka 15 iliyopita!

Mstaafu wetu pia ana tarakimu za kadi ya Nida, sio kadi yenyewe, aliyoiomba miaka sita iliyopita, lakini akakata tamaa na kuamua kubaki na namba tu, alipojikuta akilazimika kuchapa lapa la kizee kwenda kwenye ofisi zao kama mara tano kwa nyakati tofauti na kuambiwa kwamba vyeti bado havijatoka.

Akakubali yaishe na akabaki na namba yake, ambayo amejikuta akilazimika kuiandika mara kadhaa sehemu tofauti ndani ya nyumba yake, ikiwemo ukuta wa chumbani mwake, ili asije akaisahau. Unajua tena, uzee!

Mstaafu wetu alikuwa na kadi ya chama chake pendwa cha siasa, aliyoikata wakati chama hicho kikiadhimisha mwaka mmoja tangu kuungana na chama cha Zenji, yeye akiwa ‘bitozi’ wa miaka 19 tu na ndiyo anaanza kudunda mzigo miaka hiyo ya mwishoni mwishoni mwa 70′.

Ndio, miaka 15 iliyopita akastaafu kwa hiari, ili kuangalia mambo mengine ya maisha akiwa na nguvu, kuepuka yale yaliyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu kwamba unapokuwa kijana unaweza kwenda kokote unakotaka, lakini ukiishakuwa mzee unakuwa mtu wa kuongozwa na kushikwa mkono na kupelekwa hata usikotaka!

Akastaafu huku mapenzi yake kwa chama chake pendwa cha siasa na Haki yake ya kupiga kura vikistaafu pamoja naye. Akastaafu na kuwaachia vijana, naye kubaki na Utanzania wake na kadi yake ya ustaafu kutoka ile kampuni kubwa ya ‘naniliu’!

Lakini miaka ilivyosonga mbele, ndivyo thamani ya kadi yake ya ustaafu ilivyozidi kuporomoka, hata kufikia mstaafu kukosa huduma muhimu kwa kuonesha kadi ya ustaafu ya kampuni ‘naniliu’ pale alipotakiwa kujitambulisha, licha ya kuonekana wazi kuwa ni mdingi!

Yaani, kadi yake ya ustaafu kutoka kampuni ‘naniliu’, iliyokuwa mashuhuri enzi zake na kumuajiri wakati ikishiriki kikamilifu kuijenga nchi, sasa ilikuwa si chochote si lolote mbele ya vitambulisho vya kumtambulisha vilivyotengenezwa miaka sita tu iliyopita! Kweli, Burundi ilikuwa inamhusu mstaafu!

Mstaafu amepitia mitandao ya kijamii na anaona hapa na pale vijana kwa wazee wakirudisha kadi za vyama vyao pendwa kwa sababu hizi na zile ili viongozi wa vyama vyao pendwa wawasikilize. Ni jambo jema…

Mstaafu sasa anapokea pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi, lakini miezi mitano tu iliyopita alikuwa akipokea shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi kwa miaka 21 iliyopita. Sijui tuliwezaje kuishi, baada ya kuongezwa shilingi elfu hamsini kwenye pensheni yake, ambazo bado hazitoshi!

Anafikiria yeye na ‘wastaafu’ wenzake, achukue kadi yake ya ustaafu akairudishe kule kwenye kibubu kinachotunza hela zake, ambazo kinazitumia kufanya biashara, lakini faida yake anaishia kuisikia harufu tu, huku kibubu kikiahidi kumpa shilingi milioni tano na laki tano akifariki, au kitamhudumia mwenza wake wa miaka 61 akipata ujauzito! Kweli, akutukanaye hakuchagulii tusi!

0754 340606 / 0784 340606