Mzize awakosha Wafaransa Yanga | Mwanaspoti

TAARIFA njema kwa mashabiki wa Yanga kuanzia juzi ni uhakika wa mshambuliaji wa timu hiyo, Clement Mzize kusalia ndani ya kikosi hicho, lakini makocha wawili wa Kifaransa wamefungukia hatua hiyo wakisema mambo mazito.

Tuanze na yule Mfaransa Hamdi Miloud ambaye aliachana na timu hiyo msimu uliopita mara baada ya kuwaachia makombe matatu, ameliambia Mwanaspoti, Mzize kusalia ndani ya Yanga ni hatua ya kuibakisha nguvu kubwa ya safu ya ushambuliaji.

Hamdi alisema hakuna kocha ambaye anaweza kuthubutu kumuweka nje Mzize kama yuko sawa kiafya kutokana na kasi yake na akili yake ya kufunga, akisema bado timu hiyo itasumbua.

“Nilikuwa nawaza kama Aziz KI (Stephanie) aliondoka, Khalid Aucho na Clatous Chama wameondoka, kisha na Mzize akiondoka kuna kitu kikubwa kitapungua, kujenga tena nguvu kama hiyo ingehitaji muda,” alisema Hamdi anayeifundisha kwa sasa Ismailia ya Misri na kuongeza;

“Mimi nilifurahia kufanya kazi na Mzize ni kijana ambaye ana njaa ya mafanikio, usisumbuke na kupoteza nafasi lakini anaweza kufunga ndio maana unaona aliweza kufikisha mabao 14.

“Kuna wakati alikubali kucheza hata akiwa na maumivu, hata ukimwambia pumzika anakwambia kocha nitacheza, nadhani anaweza kuwa bora zaidi msimu ujao ni hatua nzuri kwa Yanga.

Wakati Miloud akisema hiyo mrithi wake ndani ya Yanga, Romain Folz naye amechekelea hatua ya kubaki kwa mshambuliaji huyo akisema safu yake ya ushambuliaji imesalia na silaha muhimu.

Folz ambaye anakwenda kuanza msimu wa kwanza alisema bado anaamini mshambuliaji huyo hajaua ndoto zake za kwenda kucheza nje ambapo sasa atakwenda kujiongezea thamani kubwa.

“Ni taarifa nzuri kwa klabu kubaki na mchezaji kijana kama huyu ambaye nishati yake ni kubwa uwanjani, nadhani bado anaendelea kujifunza na kujiimarisha kwenye safari ya kuwa mchezaji mkubwa,” alisema Folz na kuongeza;

“Sidhani kama ni uamuzi mbaya kuamua kubaki hapa, ukiangalia umri wake anaendelea kukuwa vizuri, kitu muhimu hapa kama atakuwa na muendelezo atajiongezea thamani kubwa.”

Mzize msimu uliopita alifanikiwa kumaliza na mabao 14 akiwa mshambuliaji pekee aliyefunga mabao mengi ndani ya msimu huo kwa Yanga na wazawa kwa ujumla, akifuatiwa na Prince Dube aliyefunga mabao 13.