Nishati safi yapigiwa chapuo usafiri wa ardhini

Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi ikishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imetangaza kaulimbiu ya nishati safi na ubunifu katika usafirishaji kuelekea katika maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Usafirishaji Endelevu wa Ardhini nchini.

Madhimisho hayo ya mara ya kwanza yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 24 hadi 29 mwaka huu.

Hata hivyo kaulimbiu ya mwaka huu wa kwanza inasisitiza umuhimu wa mifumo ya usafiri endelevu yenye kuchangia katika malengo ya maendeleo endelevu ya dunia (SDGs).

Hatua hii inakuja ikiwa ni mwitikio wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa Mei 16, 2023 kupitia uamuzi namba 77/286, ulioanzisha Siku ya Usafiri endelevu duniani (World Sustainable Transport Day) ambayo huadhimishwa Novemba 26 kila mwaka.

Akizungumza leo Agosti 29, 2025 na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema maadhimisho hayo yataleta pamoja wadau wa sekta ya usafiri wa ardhini kutoka ndani na nje ya nchi ili kujadili namna ya kuboresha mifumo ya usafiri salama, shirikishi na rafiki kwa mazingira.

“Maadhimisho hayo yatakuwa na midahalo ya kisera, makongamano, maonesho na majadiliano ya kitaalamu yatakayojumuisha sekta binafsi, taasisi za kiserikali, jumuiya za kikanda na kimataifa pamoja na wadau wa usafirishaji barabara, reli na waya,” amesema Suluo.

Kwa mujibu wa ratiba, kilele cha maadhimisho hayo inatarajiwa kufanyika Novemba 29, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Amesema maadhimisho hayo pia yanatajwa kuendana na juhudi za serikali za kukuza matumizi ya nishati safi katika usafiri, ikiwemo miradi ya mabasi ya mwendokasi yanayotumia gesi asilia (CNG), pamoja na magari ya umeme yanayoanza kuingia sokoni.

Kwa mujibu wa Suluo, lengo kuu ni kuwaleta pamoja wadau wote wa sekta ya usafiri wa ardhini na kuunda malengo ya pamoja ya utekelezaji, ili huduma ya usafirishaji iboreshwe, iwe salama, rafiki kwa mazingira na yenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za reli, Benjamin Mbimbi amesema tayari Tanzania imeanza kuona manufaa ya kutumia nishati safi katika mradi wa reli ya kisasa (SGR).

“Kwa sasa SGR inatumia umeme badala ya dizeli, hii imepunguza gharama za uendeshaji kwa zaidi ya asilimia 65 na pia imepunguza athari za uchafuzi wa mazingira. Tuking’ang’ania mafuta tungepoteza fedha nyingi na kuendelea kuchafua mazingira,” amesema Mbimbi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani amesema sekta ya usafirishaji imefarijika kupata siku maalumu ya kutambua mchango wake.

“Sekta hii ni kubwa, ni kama tembo, kwa muda mrefu tumekuwa hatuna siku yetu sasa tunafarijika. Serikali kuleta gesi kama mbadala wa mafuta ni hatua kubwa. Tunashauri pia kuanzishwa kwa carbon tax kwa wanaotumia mafuta ili kulinda mazingira na kuongeza mapato ya taifa,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus Joseph amesema dunia inaelekea kupunguza matumizi ya mafuta hivyo na wao hawatakiwi kubaki nyuma.

“Tayari tumeshuhudia mabasi ya umeme yakifanya safari kwa gharama nafuu ukilinganisha na yale yanayotumia mafuta. Kwa mfano, basi la umeme linaweza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa gharama ya umeme ya takribani Sh15,000, wakati basi la dizeli hutumia zaidi ya Sh300,000 kwa safari moja. Hii itasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kutunza mazingira,” amesema Joseph.

Pia, amesema kuwa ushiriki wa wadau kwenye wiki hiyo utatoa nafasi ya kujifunza teknolojia mpya na namna bora ya kupunguza gharama za uendeshaji.