Nondo za CUF kwa elimu ya Tanzania

Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini wamechambua ilani ya uchaguzi ya Chama cha Wananchi (CUF) ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 inayotoa dira ya kina juu ya sekta ya elimu nchini Tanzania wakisema ina mambo mazuri, tatizo ni ahadi kutotekelezwa.

Ilani hiyo inaeleza mikakati ya kuhakikisha elimu bora, jumuishi na yenye tija kwa Watanzania wote katika kipindi cha miaka mitano (2025 hadi 2030).

Katika ilani hiyo, neno elimu limejitokeza mara 192, jambo linaloashiria kuwa CUF inaona elimu ni msingi wa maendeleo ya Taifa na njia ya kumfanya kila Mtanaznia awe na uwezo wa kuendeleza maisha yake na biashara.

Hii inaashiria sera yenye malengo makubwa ya kijamii na kiuchumi, ikijumuisha kila kipengele cha maisha ya kijamii, kuanzia elimu ya awali hadi ya juu, ufundi, elimu kwa watu wenye ulemavu na ya watu wazima.

Mwalimu Samson Sombi, mdau wa elimu anasema ahadi katika sekta ya elimu kupitia ilani hiyo ni nzuri, lakini uzoefu unaonyesha ilani nyingi za vyama mambo mengi mazuri yanawekwa kando.

“Kuzungumzia masuala ya elimu ni jambo jema lakini utekelezaji ni la muhimu zaidi, unapoboresha makazi, kuwapatia walimu vitendea kazi bora utakuwa umenyanyua morali yao ya kufanya kazi kwa ubunifu,” anasema.

Sombi anasema ni vema vyama vya siasa vimetambua umuhimu wa elimu kupitia ilani zao kwani wameonyesha ni namna gani elimu ya Tanzania inapaswa kujengewa misingi imara, si tu kupitia mitalaa, bali kuwapo utashi wa kisiasa.

Mdau wa elimu, Ochola Wayoga anasema yanayoelezwa na CUF siyo mapya, tayari Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliyaainisha kwenye ilani yake.

“Jambo la muhimu ni uboreshaji wa maisha ya walimu wafanye kazi zao kwa uweledi, wasiwe wanateseka. Kwa walimu kutofanya kazi nyingine si tatizo, madaktari wanafanya kazi zao na wanafanya kazi zingine kwa muda wa ziada,” anasema.

Wayoga anasema CUF kwa ajenda yake itaongoza uwezo wa watu kuelewa mambo ya uchaguzi na kumchagua kiongozi anayeweza kuwa mwakilishi wa wananchi.

Mchambuzi wa masuala ya elimu, Magabilo Masambu anasema changamoto iliyopo ni idadi kubwa ya Watanzania au watoto kuwa wengi darasani, hivyo uboreshaji wa miundombinu ya elimu unapaswa kuwa kipaumbele.

“Ili elimu iwe bora lazima iwafae watu na siyo kuwapeleka mbele, sasa ukisema unaboresha mitalaa ni ipi? tunataka elimu ambayo si ya mtu kusoma na kujibu mitihani,” anasema.

Masambu anasema tatizo ambalo Serikali iliona kwenye sekta ya elimu ni wahitimu kukosa ujuzi ndiyo maana ikaja na elimu ya amali.

Anasema kama CUF imedhamiria kuifanya elimu ya Tanzania kuwa ya vitendo zaidi, basi itakuwa inasukuma mbele ajenda ya Serikali ya kuifanya elimu kuwa bora zaidi tofauti na ilivyo sasa.

“Kama wanataka kuboresha elimu lazima waboreshe mfumo mzima, kila hatua ambayo mwanafunzi akimaliza elimu yake asiwaze kuajiriwa bali aajiriwe,” anasema.

CUF kinajinasibu kuwa kinatambua hali ya sasa ya elimu nchini ina changamoto kubwa. Kinasema asilimia 30 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wamedumaa, hali ambayo inadhihirisha tatizo la upungufu wa huduma za awali za elimu na lishe bora.

Watoto wengi wanahudhuria shule lakini hawapati elimu bora, huku uhaba wa walimu wenye sifa, miundombinu duni na vifaa vya kufundishia vikiwa kikwazo kikubwa.

Hali hii inasababisha kiwango cha chini cha ufaulu, zaidi ya nusu ya wanafunzi hawapati alama za kufaulu mwaka hadi mwaka.

Masilahi duni kwa walimu, malimbikizo ya posho na mishahara midogo, vinachangia wajihusishe na shughuli za kujikimu badala ya kufundisha kwa weledi, hali inayoporomosha ubora wa elimu kwa ujumla.

Ilani inaweka mkazo maalumu katika elimu ya awali. CUF inalenga kufanya elimu ya awali (chekechea) kuwa ya lazima na bure kwa watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano.

Mpango huo utahusisha utoaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kuandaa walimu wenye sifa kupitia programu maalumu na kuboresha miundombinu ya shule kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa kijamii.

CUF inapanga kuondoa kodi zote zinazotozwa kwa shule za awali na vifaa vyake, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa elimu ya awali kwa watoto wote bila kikwazo cha kifedha.

Elimu ya msingi pia inashughulikiwa kwa kina. CUF inalenga kuhakikisha elimu hiyo ni bure, bila ada au michango isiyo rasmi. Serikali itatoa vitabu, vifaa vya kufundishia na huduma muhimu zote.

Ili kudumisha afya na utendaji wa wanafunzi, CUF inapanga utaratibu wa kitaifa wa lishe shuleni, kuhakikisha kila mwanafunzi anapata angalau mlo mmoja kamili kwa siku.

Kupunguza msongamano darasani kutafikiwa kwa ujenzi wa madarasa mapya na ajira ya walimu wa kutosha ili kuhakikisha uwiano mzuri kati ya walimu na wanafunzi.

Mabadiliko ya mitalaa yatazingatia mbinu za kufikiri kwa kina, utatuzi wa matatizo, stadi za maisha na ujuzi wa Tehama. Pia, kuimarisha ufundishaji wa Kiingereza bila kuathiri Kiswahili, hali inayolenga kutoa msingi thabiti kwa shule za sekondari na elimu ya juu.

Sekta ya elimu ya sekondari, ingawa ilipewa umuhimu, bado inakabiliwa na changamoto kama uhaba wa walimu wenye sifa, vifaa vya maabara, vitabu, maktaba na ongezeko la wanafunzi kuliko miundombinu iliyopo.

CUF inapanga elimu ya sekondari kuwa njia ya umahiri na ujasiriamali, kuhakikisha elimu inatolewa bure na bila michango ya aina yoyote, pamoja na kuanzisha vituo vya elimu ya ufundi kwa kila wilaya.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila kijana anayemaliza elimu ya msingi akakosa nafasi ya kuendelea na sekondari, anapata fursa ya kujiajiri kupitia elimu ya ufundi na stadi zinazohitajika kwenye soko la ajira.

Chama hicho kinasema miundombinu ya shule itarekebishwa ili kuondoa vikwazo, walimu watafundishwa stadi maalumu, huku gharama za masomo na vifaa vya kujifunzia na waangalizi zitatimizwa kwa asilimia 100.

“Elimu ya watu wazima, ambayo imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kupungua kwa rasilimali na darasa za usiku itarejeshwa na kuimarishwa,” inaeleza ilani ya CUF.

Kinasema kinalenga kurejesha madarasa ya watu wazima katika kila shule ya msingi, kutoa maktaba za kisasa zisizo na ada, kuunganishwa na intaneti na kufanya kazi kwa saa nyingi ili kuhamasisha utamaduni wa kujisomea na kujieleza kielimu katika maisha yote.

Kinajinasibu kuwa programu hizo zinatambua elimu si mwendelezo wa watoto tu, bali ni chombo cha maisha kwa kila Mtanzania.

CUF kinapanga kuingiza teknolojia ya akili mnemba (AI) katika mitalaa, kuimarisha ujuzi wa walimu, kuboresha miundombinu ya Tehama na kuanzisha vituo vya utafiti na ubunifu wa AI katika vyuo na taasisi za elimu.

Hatua hizo zinalenga kuandaa vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali, kukuza ubunifu wa ndani na kutatua changamoto za Taifa kupitia maarifa ya kisasa.

Chama hicho kinasema kinatambua umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi, ya fedha na ya jamii.

Kinasema mpango wa taifa wa elimu ya fedha na soko la hisa utahamasisha uelewa miongoni mwa wananchi, vijana, wanawake na wajasiriamali.

Kampeni za elimu ya afya ya uzazi na kupambana na mimba za utotoni zinatarajiwa kuimarisha uelewa wa jamii, huku ikitoa motisha kwa familia zenye kipato cha chini kuhakikisha watoto wa kike hawaachi shule.

Vilevile, wavuvi na wadau wa sekta ya uvuvi watapata mafunzo ya vitendo kupitia vyuo maalumu vya ufundi wa uvuvi na ufugaji wa majini, huku Tehama ikitumika kuwahamasisha wavuvi kuhusu uvuvi wa kisasa, usalama majini, uhifadhi wa mazingira na masoko.

Kuhusu ajira na uchumi wa wajasiriamali, CUF inalenga kuhakikisha elimu inawawezesha vijana na wananchi kuwa na stadi zinazohitajika, kutoa ujuzi wa ufundi, sayansi, teknolojia, ujasiriamali na akili mnemba.

CUF imeahidi bajeti ya elimu itatengwa si chini ya asilimia 25 ya bajeti ya Taifa kila mwaka na asilimia 50 ya bajeti hiyo itahusu elimu ya awali na msingi.