Omary achekelea kurudi nyumbani | Mwanaspoti

BAADA ya kuanza kuitumikia Mashujaa kwa mkopo akitokea Simba, kiungo Omary Omary amefurahia kurudi nyumbani na kukutana na ushindani mkubwa akiamini kwamba amefanya uamuzi sahihi kurejea katika timu hiyo aliyoichezea kabla ya kutua Msimbazi msimu uliopita.

Omary amefunguka hayo siku moja baada ya timu yake kuambulia suluhu dhidi ya Al Hilal katika mechi ya kirafiki iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Omary alisema amerudi timu iliyomlea na kumpa nafasi ya kuonekana na amefurahishwa na kukutana na mabadiliko makubwa ya kikosi ambacho amekitaja kuwa ni bora na cha ushindani.

“Ni mapema sana kufahamu kama nitacheza kikosi cha kwanza, ndio kwanza nimerudi na nimekuta wachezaji wengi bora hivyo napambana kuonyesha ili kocha yeye ndio aamue nani aanze na nani amsubiri mwenzie benchini,”  alisema Omari ambaye akiwa Simba alishindwa kabisa kuonyesha makeke na kuishia kukaa benchini muda mrefu wa msimu uliopita.

“Kiujumla Mashujaa wametimia ina kikosi kizuri na bora naamini muda ndio utakaoongea msimu ukianza nafurahishwa na ushindani unanipa hali ya kupambana na kuonyesha nini natakiwa kukifanya.”

Omary alisema mechi za kirafiki wanazocheza zinawapa picha ni namna gani wanatakiwa kujipanga kuelekea msimu ujao wakizingatia hawatakuwa na kazi rahisi kupambania timu hiyo iweze kufanya vizuri.

“Kocha ametupima kwenye mechi nne sasa na tumeweza kufanya vitu sahihi na amekuwa akitukumbusha wajibu wetu pale tunapokosea nafikiri ni wakati sahihi sasa na sisi kuipigania nembo ya timu hii kutokana na uwekezaji uliofanyika.”

Omary amerudi Mashujaa kwa mkopo baada ya kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Simba chini ya kocha Fadlu Davis akiambulia kucheza mchezo mmoja kati ya 30 ya msimu mzima.