BAADA ya kuwa na kambi ya wiki mbili mkoani Morogoro, Pamba Jiji Jumatatu ijayo inatarajia kwenda Kenya kupiga kambi ya muda mfupi sambamba na kucheza mechi tatu za kirafiki kabla ya kurudi Tanzania tayari kwa ushindani wa Ligi Kuu Bara.
Pamba Jiji ambayo imetoka kuifunga Fountain Gate mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki na leo inarudi Mwanza kupumzika kwa siku mbili kabla ya kuanza safari Jumatatu kufuata mechi hizo tatu za kirafiki.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Pamba, Francis Baraza alisema yeye ndiye atakayeipokea timu hiyo nchini humo baada ya kutangulia siku tatu zilizopita kutokana na kupatwa na msiba wa baba mzazi.
“Ni kweli timu itakuja huku nami nipo huku nina siku mbili zaidi nimerudi kumzika baba aliyefariki dunia, nilipata taarifa nikiwa Morogoro kambini nimepata ruhusa na kuja kumpumzisha na nilikuwa na ratiba ya kuja huku kwa mechi tatu za kirafiki,” alisema Baraza na kuongeza;
“Timu itakuja huku Jumatatu na tutacheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya Mara Sugar, Home Boys na Shabaha zote zinashiriki Ligi Kuu Kenya lengo la kufanya hivi ni kuiweka timu tayari kabla ya mchaka mchaka wa Ligi Kuu Bara.”
Baraza alisema ni kipimo sahihi kwao kucheza mechi hizo kabla ya msimu kuanza baada ya kufanya mazoezi kwa muda na kufanikiwa kucheza mechi moja ya ndani kama mazoezi dhidi ya Fountain Gate wanaamini mechi hizo ni kipimo sahihi kwao.
Pamba inashiriki Ligi Kuu kwa msimu wa pili tangu ilipopanda msimu uliopita baada ya kuisotea miaka 23.