Raia wa Kigeni Akashutumiwa Baada ya Kumnywesha Tembo Bia – Global Publishers



Mamlaka nchini Kenya zimeanza uchunguzi dhidi ya raia wa Uhispania aliyenaswa kwenye video akimnywesha tembo bia katika hifadhi ya kibinafsi ya Ol Jogi Conservancy, Kaunti ya Laikipia. Video hiyo, iliyosambaa mitandaoni wiki hii, ilionesha mgeni huyo akimimina bia aina ya Tusker kwa tembo maarufu anayejulikana kwa jina la Bupa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Wanyamapori Kenya (KWS), kitendo hicho hakikubaliki na ni kinyume cha kanuni za uhifadhi. Msemaji wa KWS, Paul Udoto, alieleza kuwa mtu huyo hutumia jina la Skydie_Kenya kwenye mitandao ya kijamii na tayari ameanza kufuatiliwa.

“Hatua kali zitachukuliwa. Sisi haturuhusu mtu yeyote kupeleka chakula au vinywaji kwa wanyama. Tukio hili linaonyesha dharau kubwa kwa sheria za uhifadhi,” alisema Udoto.

Wahifadhi kutoka hifadhi ya Ol Jogi walishutushwa na video hiyo. Mfanyakazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina Frank alisema:

“Hii haikupaswa kutokea. Sisi ni wahifadhi na jukumu letu ni kuwalinda wanyama, siyo kuruhusu mambo kama haya. Hata kuwakaribia tembo ni hatari, sembuse kuwanywesha pombe.”

Wakenya wengi mitandaoni walikerwa na kitendo hicho, wakidai ni udhalilishaji wa taifa na urithi wake wa wanyamapori. Baadhi walitaka raia huyo afukuzwe nchini, huku wengine wakisema video hiyo inaweza kuathiri taswira ya Kenya kama kituo cha utalii kinachoheshimu uhifadhi.