Sababu Fei Toto kumficha mpenzi

KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni msiri mkubwa katika sekta ya mahusiano na mwenyewe amefunguka sababu ya kufanya hivyo.

Fei Toto alisema ameamua kufanya hivyo ili yasiingiliane na kazi yake ya kucheza mpira.

“Kiukweli ni mpenzi yupo, lakini huwa sipendi kuweka uhusiano wangu hadharani, kazi  yangu haihusiani kabisa na ishu zangu hizo, hayo ni maisha yangu binafsi,” alisema Fei Toto aliyekuwa katika jukumu la kuitumikia Taifa Stars katika fainali za CHAN 2024 zilizopo mwishoni zikiandaliwa kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

“Hata mwenyewe niliyenaye huwa hapendi hata kutokea kwenye mitandao au magazetini,”  Fei alifafanua zaidi.

Hii imekuwa tofauti na baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa wakiweka wazi mahusiano yao.

Hivi karibuni nyota huyo wa zamani wa JKU na Yanga, alisaini mkataba wa nyongeza wa mwaka mmoja, utakaomfanya asalie kubaki Azam hadi 2027 ikiwa alibakiza mkataba wa mwaka katika timu hiyo na kuzima tetesi za kuibukia Simba na Yanga zilizokuwa zikitajwa kumnyemelea.