Samia, Dk Nchimbi wanavyoanza kuzisaka kura mikoani

Kampeni za wagombea urais na mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi (CCM) zinaendelea leo Ijumaa, Agosti 29, 2025 katika maeneo tofauti nchini.

Wakati, mgombea urais, Samia Suluhu Hassan akiwa mkoani Morogoro, mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi ataanza kuchanja mbuga mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye wapigakura wengi, akianzia Mwanza.

Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na orodha ya Daftari la Kudumu la Wapigakura, Kanda ya Ziwa ndiyo yenye idadi kubwa ya wapigakura.

Chama hicho tawala kitaendelea kunadi ilani ya uchaguzi mkuu 2025/2030 baada ya jana Alhamisi, Agosti 28, kuzindua kampeni kitaifa katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na umati wa makada wa chama hicho, wakiwemo viongozi wenye hadhi na nafasi mbalimbali kwenye chama pamoja na wastaafu.

Katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro alisema maandalizi nchi nzima kwa ajili ya kampeni za chama hicho yamekamilika na wagombea wao watashuhudia watakapofika huko.

Dk Migiro alisema maelekezo ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia ni kwamba maandalizi yafanyike na waendeshe kampeni za kistaarabu kwa ngazi zote za udiwani, ubunge na urais.

Rais Samia alisema uzinduzi wa kampeni hizo ni mwanzo wa safari yao ya kwenda kwa wananchi kuomba ridhaa ya kuendelea kuwatumikia.

“Tunatoka kwenda kwa wananchi kwa sababu kuu mbili; moja, tumetekeleza kwa mafanikio makubwa Ilani ya CCM 2020 hadi 2025 ikiwemo kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” alisema Rais Samia na kuongeza:

“Pili, CCM kwa umadhubuti, kuaminika kwake, utendaji wake na historia yake ni nguzo muhimu kwa utumishi na mustakabali wa Taifa letu.”

Kampeni za uchaguzi mkuu zimeanza Agosti 28 zitaendelea hadi Oktoba 28. Siku ya Jumatano ya Oktoba 29 itakuwa upigaji kura.

Ratiba ya INEC kwa CCM inaonyesha, Rais Samia akitoka Morogoro atakwenda Dodoma, Songwe, Mbeya na maeneo mengine.

Kwa upande wa Dk Nchimbi aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, akitoka Mwanza atakwenda Mara, Simiyu, Shinyanga na Geita.

Katika mikoa hiyo watafanya mikutano midogomidogo na mikubwa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

CCM wako kwenye mbio hizo  wakichuana na vyama vingine 17 kwa nafasi ya urais, ambavyo bado havijazindua kampaeni zake,  licha ya ratiba kuonyesha baadhi vinapaswa kuwa vimeanza.