Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mvomero kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Sara Msafiri, amesema historia ya migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji katika wilaya ya Mvomero sasa imefutwa kabisa, kufuatia juhudi kubwa zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM na Mgombea Urais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizunguza kwenye mkutano wa kampeni mjini Morogoro, Bi. Sara amesema migogoro hiyo ilifika hatua ya wananchi kuchimba mitaro ili kutenganisha mipaka kati ya wakulima na wafugaji, hali iliyosababisha majeruhi na uharibifu wa mali kwa muda mrefu.
“Wananchi wa Mvomero mnakumbuka tulivyoteseka kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Wakulima walilazimika kuchimba mitaro ili kuzuia mifugo isiingie mashambani mwao, hali ambayo ilisababisha taharuki na kutoelewana baina ya jamii hizi mbili. Lakini tunamshukuru Mwenyezi Mungu na tunampongeza Rais wetu, Mwenyekiti wa CCM na Mgombea Urais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua kubwa alizochukua. Leo hii changamoto hiyo imekwisha kabisa,” alisema.
Bi. Sara amebainisha kuwa amani na mshikamano vilivyorejeshwa na serikali vimewapa wananchi wa Mvomero nafasi ya kuendelea na shughuli za kilimo na ufugaji bila hofu, jambo linaloongeza tija na kukuza uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.
Pia ameongeza kuwa serikali ya CCM kupitia uongozi wa Dkt. Samia imefanya kazi kubwa katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo elimu, maji, afya na mawasiliano.
Amesema miradi ya maji imesaidia kupunguza adha kwa kina mama na watoto, maboresho ya shule yameongeza ufaulu, huduma za afya zimeimarika na mawasiliano yamekuwa ya uhakika hata vijijini.
“Haya yote ni matokeo ya uongozi thabiti wa Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunapaswa kumuenzi kwa vitendo kwa kumpa kura nyingi za ushindi, pamoja na kuwapigia kura wagombea wa ubunge na udiwani kupitia CCM,” alisema Bi. Sara.