Tanzania kudhibiti kemikali hatari za dawa za kulevya

Nashville. Tanzania imeingia makubaliano na nchi zinazozalisha kwa wingi kemikali bashirifu zinazotumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya ili kupunguza athari kwa vijana.

Hayo yamesemwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo ambaye ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya (IDEC39) nchini Marekani.

Lyimo amesema Tanzania imenufaika kwa kiwango kikubwa kutokana na ushiriki wake kwenye mkutano huo uliowakutanisha viongozi wakuu wa mamlaka za udhibiti wa dawa za kulevya kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Amesema kupitia mkutano huo ujumbe wa Tanzania umepata uzoefu kutoka wa nchi zinazotengeneza vifaa vya kisasa vya kubaini dawa za kulevya, jambo litakalosaidia kuimarisha udhibiti na usalama katika mipaka.

“Tumekumbushwa umuhimu wa kuwekeza katika upelelezi wa kisayansi. Dunia kwa sasa inashuhudia mbinu mpya za kutengeneza dawa za kulevya, ambazo zinapita nje ya mifumo ya kawaida, hali inayotishia ufanisi wa mbinu za zamani za udhibiti,” amesema Lyimo.

Mkutano huo uliofanyika kwa siku tatu kati ya Agosti 26 hadi 28, 2025 ulienda sambamba na vikao mahususi na warsha maalumu za teknolojia ya kisasa ya kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya duniani, ambayo kwa sasa inatajwa kuhamia katika majukwaa ya kidijitali.

“Hii ina maana kwamba, uwekezaji katika teknolojia na sayansi ni muhimu zaidi ili kuendelea kufanikisha vita hii. Kupitia mkutano huu, Tanzania imepata ushirikiano mpya na nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa.

“Mojawapo ya mafanikio ni makubaliano na shirika kubwa la kimataifa la INL, ambalo limeahidi kushirikiana na DCEA kupambana na dawa za kulevya, kwa kutumia vifaa vya kisasa hususani kuimarisha uchunguzi na upelelezi wa kisayansi wa kiintelijensia.

Kando na hilo, Tanzania imepata nafasi ya kujadiliana na nchi zinazozalisha mmea wa kratom unaotengeneza dawa mpya ya kulevya aina ya Mitragyna Speciosa na kuridhiana njia bora ya kushirikiana kudhibiti dawa hiyo inayotajwa kuwa tishio kwa sasa.

Agosti 13 mwaka huu mamlaka hiyo ilikamata tani 18.5 za shehena ya dawa za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa zikiwa zimeingizwa nchini Tanzania kama mbolea, kwa ajili ya bustani za mbogamboga na maua.

Hiyo haikuwa  mara ya kwanza kwa aina hiyo mpya ya dawa za kulevya kukamatwa Tanzania, b aada ya Juni 2025 kukamata kontena lenye futi 40 likiwa na shehena ya tani 11.5 ya dawa hizo, zikiwa zimefungashwa kwenye mifuko 450 kwa jina la mbolea.

Dawa hiyo inatajwa kuwa na madhara sawa na dawa za kulevya jamii ya afyuni, ambazo ni heroini na morphine, kwani huathiri mfumo wa fahamu pamoja na kusababisha uraibu na vifo vya ghafla.