Dar es Salaam. Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), kinatarajia kuzindua kampeni zake Septemba 4, 2025 huku kikiahidi kuwa zitafanyika kwa amani na utulivu.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Agosti 29, 2025 na mgombea urais wa chama hicho, Yustas Rwamugira, katika hafla ya wananchama kumpokea iliyofanyika makao makuu ya chama hicho Magomeni, Dar es Salaam akitokea jijini Dodoma baada ya uteuzi.
Kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 zimeanza Agosti 28 na zinatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 28.
Vyama 17 vimethibitishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kusimamisha wagombea katika uchaguzi huo wa Rais, wabunge na madiwani.

Rwamugira amesema uzinduzi wa kampeni za TLP utafanyika katika viwanja vya Manzese na baada ya hapo zitaendelea kwa miezi miwili mfululizo na kuhitimisha mkoani Arusha.
“Baada ya kutua hapa, ndiyo kazi ya kampeni inaanza, katika kipindi chote tunaahidi kufanya kampeni za amani na utulivu, tunawakaribisha wananchi wote kuja kusikiliza sera zetu,” amesema.
Amesema kipaumbele cha kwanza cha chama hicho kwenye sera ni utulivu na amani, cha pili ni utawala bora unaofuata sheria na haki.
Rwamugira amesema wanaamini kwa kufanya hayo, mambo mengine muhimu yataweza kutekelezeka.
Mgombea mwenza wa chama hicho, Amana Suleiman Mzee, amesema endapo chama hicho kitashika dola, moja ya kazi kubwa watakayofanya ni kufuta mikopo maarufu kausha damu inayowadhalilisha wanawake.
“Chama chetu hakitakubali mikopo kausha damu inayowadhalilisha wanawake huko mitaani iendelee endapo tutashika dola, pia tutahakikisha kunakuwapo huduma bure za afya kwa wanawake na watoto,” amesema na kuongeza:
“Hivyo naomba wanawake mjitokeze kwa wingi kusikiliza sera zetu na itakapofika siku ya uchaguzi mtuchague kwa kuwa hatutawaangusha katika kuwaletea maendeleo.”
Awali, Katibu wa Uenezi wa TLP, Bakari Makame amesema katika uchaguzi wa mwaka huu jambo la kufurahisha ni idadi kubwa ya wanawake wamejitokeza kugombea kulinganisha na wanaume.
Kutokana na hilo, amewataka wananchi kuwaunga mkono wagombea wa chama hicho na kuondoa dhana potofu kuwa wanawake hawawezi kuongoza.
“Naomba wananchi waondokane na dhana kuwa wanawake hawawezi kuongoza kwani mifano tunayo kwa Samia Suluhu Hassan, Rais anayemaliza muda wake na sasa anagombea, hivyo tunaomba muwaunge wagombea wetu mkono kwa kuwapigia kura,” amesema.
Amesema TLP imejipanga kushiriki kikamilifu uchaguzi kwa kusimamisha wagombea katika kila jimbo, kata na uwakilishi Zanzibar, kikijinasibu kwa kaulimbiu: “Kaza buti, barabara ina kokoto.”
Makame amesema maandalizi ya chama hicho yanaonyesha safari ya kuelekea kushika dola inawezekana.
“Sasa tunawaambia kweli kwamba tumejipanga. Tumeweka wagombea kila jimbo, kila kata na hata kwenye uwakilishi. Tunachofurahia zaidi ni kwamba idadi ya wagombea wanawake imekuwa kubwa kuliko wanaume, jambo linalotupa matumaini makubwa. Tunaamini kushika dola inawezekana,” amesema.
Kwa zaidi ya saa mbili wanachama wa TLP wamemsubiri mgombea huyo wa urais na mgombea mwenza kuwasili katika ofisi za makao makuu ya chama hicho.

Wawili hao waliwasili wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeusi waliyopewa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na kulakiwa na wanachama waliokuwa wameshika bendera, wakiimba nyimbo za chama hicho.
Baada ya kumpokea hatua chache kutoka zilipo ofisi za makao makuu ya chama hicho, alisimama kwa muda nje na kuzungumza na waandishi wa habari, kisha akaingia ndani ya ofisi ambako kulifanyika kikao.