Uchaguzi wa viongozi wa Serikali na Bunge ni tukio la kisiasa lenye athari za moja kwa moja kwa mustakabali wa fedha na mazingira ya uwekezaji, na hata uchumi kwa ujumla. Ni jambo la kujivunia kuwa kunakuwapo na uchaguzi katika Taifa, na kipindi hiki ni wakati mwafaka wa kusikiliza na kuchambua sera za vyama mbalimbali.
Uamuzi wa kisiasa unaopitishwa kupitia sera za vyama hayana tu athari za muda mfupi bali huamua mwelekeo wa miaka mingi mbele kwenye uchumi wa taifa husika. Chama kinachoshinda uchaguzi kinapata ridhaa ya kutekeleza sera zake na hivyo kuwa na athari kwenye bajeti ya serikali, mzunguko wa fedha na kwenye njia mbalimbali za matumizi ya rasilimali kwenye kuboresha maisha ya watu na ukuaji wa kiuchumi.
Wakati wa harakati za uchaguzi, pengine ndio muda ambao kunakuwa na mzunguko wa kifedha kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, yawe ya mijini na vijijini. Hii ni kwa sababu, ni wakati wa wagombea kunadi sera za vyama vyao na wagombea wao.
Hivyo kunakuwa na mahitaji mbalimbali kufanikisha haya ikiwamo mahitaji ya huduma mbalimbali kama malazi na vyakula, vyombo vya muziki na aina nyingine ya huduma za kuwezesha kufanikisha shughuli za kampuni na upigaji kuwa.
Pia kunakuwa na ajira za muda mfupi ambazo zinatolewa na mamlaka mbalimbali na pia vyama na wagombea kufanikisha zoezi la uchaguzi. Ni kipindi chenye shamra shamrashamra nyingi na hivyo kuwa na ongezeko la fedha kwenye mzunguko.
Kwa kawaida chama kinachoshinda uchaguzi kinakuwa na ridhaa ya kuunda serikali na kupeleka mabadiliko ya sera na sheria bungeni na hivyo kuathiri namna serikali inavyofanya manunuzi ya umma. Kwa hivyo, matokeo ya uchaguzi yanaweza kuleta mabadiliko chanya ambayo yanachochea ukuaji wa uchumi na ajira, au kusababisha kukosa utulivu wa kifedha na kushuka kwa viwango vya uwekezaji. Hii inatokea kwenye nchi nyingi sana hasa zinazoendelea. Mabadiliko ya serikali pia huathiri ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Sera za chama kilichochaguliwa zinaweza kuvutia uwekezaji wa ndani na wa kigeni ikiwa zitatoa uwazi, uthabiti na motisha za kifedha. Mfano wa sasa ni sera zinazochochea utumiaji wa makampuni ya ndani, malighafi zinazozalishwa ndani ya nchi au kuagiza matumizi ya wataalamu wa ndani katika miradi ya umma. Hatua hizi zinaweza kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya nchi, kuongeza nafasi za kazi kwa wakandarasi wa ndani na kukuza ujuzi wa kitaalamu.
Vilevile, motisha za kodi kwa viwanda vinavyoweka mtaji, pamoja na uwekezaji wa umma katika miundombinu ya afya na elimu kupitia ushirikiano wa sekta binafsi, zinaweza kuboresha tija ya wafanyakazi na kufanya nchi kuwa kivutio kwa wawekezaji walio na mtazamo wa muda mrefu.
Pia ni vizuri kujua kuwa vyama vinakuwa na sera mbalimbali kwenye maendeleo ya kijamii kama sera za kuwawezesha vijana, wazee, na wanawake kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi kama kilimo, biashara na ujasiriamali na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, afya na mawasiliano, na hivyo kusaidia kuokoa gharama mbalimbali.
Hata hivyo, si kila ahadi au sera huleta matokeo yanayotarajiwa. Sera za kupendelea wazawa bila mpangilio wa kuimarisha ushindani, au vizingiti vya kibiashara vinavyoweka kwa haraka, vinaweza kusababisha kupungua kwa ubunifu, kuongeza gharama kwa watumiaji na kushusha ufanisi wa viwanda.
Aidha, matumizi ya fedha nyingi wakati wa uchaguzi, unaweza kusababisha mfumuko wa bei, kushuka kwa thamani ya sarafu na kuongezeka kwa gharama ya maisha. Mabadiliko ya mara kwa mara ya sera, yanaweza kuongeza hatari kwa wawekezaji hasa wakubwa na mara nyingi husababisha kuondoka kwa mitaji au kusimamishwa kwa miradi.
Wawekezaji kwa upande wao wanatafuta kuwa na uhakika wa urejeshwaji wa uwekezaji unaofanywa. Uwepo wa rekodi mathubuti ya utekelezaji wa sera, uwazi wa kifedha na mazingira thabiti ya sheria ni vitu muhimu. Kwa mfano, sera za uwazi za kodi, ardhi na mwendelezo wa sheria za biashara, mara nyingi huvutia wawekezaji.
Uwepo wa mikopo nafuu kwa wajasiriamali vijijini na programu za mafunzo ya ufundi kwa vijana vinaweza kuzaa miongoni mwao wawekezaji wadogo wadogo ambao huongeza uzalishaji wa ndani na kufungua soko la ndani kwa bidhaa na huduma mbalimbali, na hivyo kuchochea uwekezaji.
Kwa wananchi wa kawaida, kushiriki uchaguzi ni jambo la kiuchumi na muhimu sana kwani unakuwa sehemu ya mabadiliko, ama sera ambazo unatarajia zitakunufaisha. Kupiga kura ni njia ya kuchagua wale watakaoamua ni sera gani zitumike, jinsi fedha za umma zitakavyotumika, na jinsi miradi ya umma itakavyotekelezwa.
Kwa kuelimika kuhusu sera za vyama, utekelezaji na viashiria kama mabadiliko ya mtaji wa uwekezaji, uwiano wa manunuzi kwa kampuni za ndani, upatikanaji wa mikopo kwa vijana na wanawake na viwango vya mfumuko wa bei, wananchi wanaweza kutoa shinikizo kwa wagombea na taifa kwa ujumla ili kuhakikisha uwajibikaji na uwazi, na hii inawezekana kufanyika wakati wa uchaguzi.
Wakati wa kampeni, ni muhimu kuchunguza sio tu ahadi za sera bali mtazamo wa utekelezaji. Sera zinatafsiri kutokana na mpango wa maendeleo aambao utatolewa baada tu ya kuchaguliwa kwa serikali mpya.
Ni muhimu kwa wagombea na vyama kuainisha ni namna gani watakavyounda sera za kusaidia kusukuma maendeleo mbele, kwa mifano na pia kwa kuonyesha vyanzo vya fedha kugharamia sera mpya. Utekelezaji wa sera unaweza pia kuhusisha ushirikiano na sekta binafsi. Sera pia zinapaswa kuainisha namna utekelezaji utakavyosimamiwa ili kupunguza rushwa na kurahisisha ufanisi wa sera husika.
Kwa miaka mingi, na kupitia wataalamu wa fedha na uwekezaji, kuna uwiano wa wazi kati ya uchaguzi na jinsi unavyokuwa na athari kwenye uwekezaji na ukuaji wa pato binafsi la mtu mmojammoja na pia pato la taifa.
Katika nchi ambazo zimewekeza katika utengenezaji wa sera za kuvutia wawekezaji kwa uwazi na motisha za kodi, kumekuwa na maingizo ya teknolojia mpya na ajira kwa wajasiriamali. Kinyume chake, serikali ambazo zimepitisha sera za kisiasa zinazolenga mafanikio ya muda mfupi bila mipango ya kifedha zimekumbana na kushuka kwa uwekezaji, kuongezeka kwa madeni na kuporomoka kwa taasisi za kifedha.
Uchaguzi ni fursa ya wananchi kuunda mazingira ya kifedha yanayowavutia wawekezaji na kuhifadhi mustakabali wa uchumi. Pia ni wakati wa kuangalia sera zipi za kijamii zitawawezesha na kuwafaa kwa kipindi cha muhula wa uongozi wa serikali itakayokuwa madarakani.
Ni wajibu wa kidemokrasia kushiriki uchaguzi na kusoma kwa umakini ilani za vyama na pia kuuliza maswali kuhusu utekelezaji, kutafuta uwazi wa vyanzo vya fedha na kupigia kura kwa wale wanaoonyesha uwezo wa kutekeleza sera kwa uwazi na ufanisi.
Kwa kufanya hivyo, si tu tunachagua viongozi bali tunachagua njia tunayotaka taifa litumie rasilimali zake kama zitawekezwa kwa maendeleo endelevu kwa manufaa binafsi na manufaa ya ujumla ya kiuchumi ya taifa.